Habari

Teknolojia yaendesha Ramadhani mara hii

Na JURGEN NAMBEKA March 14th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

HUKU mamilioni ya waumini wa Kiislamu ulimwenguni wakiendelea na mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, baadhi wameelezea jinsi teknolojia inavyochangia kwa hali mbalimbali kufanikisha mfungo ikilinganishwa na hapo awali.

Hapo awali, Waislamu walitegemea Mwadhini msikitini, ratiba zilizochapishwa za kufunga, na hata matangazo ya vyombo vya habari ila mambo yamebadilika, kisa kikiwa ni teknolojia.

Waumini sasa wanaweza kufuatilia ratiba hizo za Mwezi Mtukufu kupitia kwa rununu zao, appu za kuonyesha saa za kufunga, na vilevile, mahubiri na mafunzo ya kidini kupitia kwenye mitandao ya kijamii kando na mbinu zile za zamani.

Sheikh Omar Buya wa Mombasa anaungama kushuhudia mabadiliko hayo moja kwa moja kwani vyombo vya kidijitali vimerahisisha jinsi Waislamu wanapokea nasaha na mwongozo wakati wa Ramadhani.

“Teknolojia imebadilisha dunia kuwa kama kijiji kidogo. Licha ya watu kuwa mataifa ya mbali, sasa wanaunganishwa na simu za mkononi.

“Kwetu sisi wahubiri imekuwa hata rahisi kutoa mahubiri wakati wa Ramadhani. Ninatoa tu mahubiri na Waisalamu kote nchini wanayapata bila taabu,” akasema Shehe Buya.

Anaongeza kuwa vijana wenye ufahamu mzuri wa kiteknolojia msikitini wamekuwa wakipeperusha mahubiri moja kwa moja wakati wa mafunzo ya ‘darasa’, huku wengine wakirekodi kwa simu zao na kisha kuyapeperusha kwenye mitandao ya kijamii.

Kando na mitandao ya kijamii, appu za simu za kusaidia waumini wasio na ratiba zilizochapishwa za kufunga, zinatumika kuwasaidia Waislamu kujua wakati wa kuanza kufunga na wakati wa kufuturu.

Aidha, appu kama vile Ramadhan Buddy, Muslim Pro na nyinginezo pia zinawakumbusha Waislamu kukariri vifungu vya Quran, kuomba na kuwasaidia waumini kufuatilia mfungo kwa mpangilio.

Kwa mujibu wa Bi Salam Athman, ambaye ni mwalimu wa Shule ya Msingi ya Mshiu iliyoko LungaLunga, Kaunti ya Kwale, teknolojia imemsaidia sana kukuza imani wakati huu wa Ramadhani.

Anaseme kuwa alifungua kundi la mtandao wa kijamii wa WhatsApp ambalo limemsaidia yeye na waumini wengine kutoka humu nchini kuungana na kutiana moyo wakati wa Ramadhani.

“Katika kundi hili huwa tunaamshana ili tufanye maombi ya asubuhi. Wengi hukimbilia simu zao wanapoamka na wanapata kukumbushwa kuwa wakati huo ulipaswa kuwa wa maombi,” asema Bi Athman.

Anaeleza kuwa kundi hilo pia hutoa makumbusho ya maombi tofauti tofauti yanayopaswa kufanywa mchana kutwa na kuwasaidia Waislamu kuwa waaminifu katika Mwezi wa Ramadhani.

“Hata mle ndani sisi hutuma video za masheikh kadhaa ili tu kukuza imani watu wasije wakaanguka katika safari ya kufunga,” akasema Bi Athman.

Bujra Mohamed wa Mwabungo kaunti iyo hiyo, mitandao ya kijamii imemwezesha kuchangisha hela za kusaidia watu wanaokabiliwa na wakati mgumu kiriziki katika msimu wa Ramadhani.

Anaeleza kuwa, teknolojia imemwezesha kufikisha ujumbe kwa wahisani wanaoishi ng’ambo, jambo ambalo halingewezekana miaka ya awali.

“Ufuasi wangu mkubwa huniwezesha kuchangisha hela za kuwapa chakula Waislamu wasiojiweza ili waweze kufuturu na wenzao. Michango pia ni ya kuboresha misikiti iliyo katika hali duni,” akasema Bw Mohamed.