Habari za Kitaifa

Serikali yakabwa kuhusu deni la Sh4.7 bilioni kwa viwanda vya sukari

Na CECIL ODONGO March 14th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

 

MUUNGANO wa Wakulima wa Miwa na Wafanyakazi wa Viwanda vya Sukari (KUSPAW) umeitaka serikali ilipe deni la Sh4.7 bilioni kabla ya mchakato wa kukodisha viwanda vya sukari kukamilishwa.

Katibu Mkuu wa Kuspaw Francis Wangara Ijumaa alisema muungano huo pia unadai usimamizi wa viwanda vya sukari vinavyomilikiwa na serikali Sh10 milioni. Pesa hizo ni makato ya wafanyakazi ambayo hayajawasilishwa kwa Kuspaw hadi leo.

Bw Wangara aliambia Taifa Leo kuwa  wamemwaandikia Waziri wa Kilimo Mutahi Kagwe kuhusu suala hilo, huku akitishia kuwa wataelekea mahakamani iwapo madeni yote wanayoyadai hayatalipwa.

“Tumemwaandikia waziri na katibu katika wizara na tumewaeleza tutapinga kukodishwa kwa viwanda hadi madeni yetu yalipwe. Hatupingi mpango wa kuvikodisha viwanda, ila tunataka wawekezaji wapya wachukue usukani tukiwa hatuwadai chochote,” akasema Bw Wangara.

“Iwapo matakwa yetu hayataridhiwa, hatutakuwa na jingine ila kuelekea kortini kuzima mchakato wa kukodisha viwanda vya sukari,” akaongeza.

Kuspaw imekuwa ikiteta kuwa haijajumuishwa kwenye kamati inayohusika na mpango unaosukwa wa kukodisha viwanda vya sukari. Imesisitiza kuwa maslahi ya wafanyakazi lazima yaangiziwe kabla ya viwanda kupokezwa wasimamizi wapya.

“Hakuna mfanyakazi atafutwa na tunataka kushirikishwa ili wawekezaji wapya wakichukua usukani, watakuwa na uhusiano imara na wafanyakazi,” akasema Bw Wangara.

Viwanda vya sukari ambavyo serikali inalenga kuvikodisha kutoka ukanda wa Nyanza na Magharibi  ni Nzoia, Sony, Chemelil na Muhoroni. Kampuni za uwekezaji zenye nia ya kutwaa usimamizi wa viwanda hivyo, zina hadi Machi 21, 2025 kuwasilisha zabuni zao.

Baada ya hapo, tenda hizo zitatathminiwa kabla kampuni zitakazoibuka bora kupokezwa usimamizi wa viwanda hivyo ambavyo vimekuwa vikilemewa na changamoto tele za kifedha.

Serikali inamiliki asilimia 98.8 katika kiwanda cha Sony, Nzoia (asilimia 97.93), Chemelil (asilimia 96.22) kisha Muhoroni asilimia 82.8.