Mauaji mengine Molo, miezi 2 baada ya kuuawa kwa mwanaharakati Richard Otieno
MIEZI miwili baada ya mauaji ya kikatili ya mwanaharakati Richard Otieno, mekanika mmoja ameuawa Elburgon eneo bunge la Molo, kaunti ya Nakuru, kwa njia kama hiyo.
Mauaji ya Godfrey Ngugi, 23, aliyetoweka mnamo Machi 9, yaliyochochea maandamano katika eneo hili wikendi na kupelekea mwanafunzi wa kidato cha tatu kuuawa kwa kupigwa risasi.
Kufuatia kisa hicho, familia mbili sasa zinaomboleza kuuawa kwa wapendwa wao.
Wakazi wa Elburgon walifanya maandamano katika barabara za mji huo wakilaani kuuawa kwa Ngugi, almaarufu FB. Mwili wake ulipatikana siku kadhaa baada ya kutoweka kwake.
Familia hiyo imekuwa ikimsaka mekanika huyo tangu alipotoweka kwa njia ya kutatanisha mnamo Machi 9 mwaka huu.
Mwili wa Ngugi ulipatikana ndani ya Mto Molo, mita chache kutoka mji wa Elburgon.
Wananchi walikabiliana na polisi wakati wa machafuko hayo, yaliyodumu kwa saa mbili, wakiwarushia mawe wakilenga kuharibu Kituo cha Polisi cha Elburgon, waliodai ni “eneo la uhalifu”.
Katika jaribio la kuwatawanya waandamanaji hao, inaripotiwa kuwa polisi walitumia risasi halide kando na vitoza machozi.
Hapo ndipo risasi moja ilipata mwanafunzi wa Kidato cha Tatu, Glen Riechi, wa Shule ya Upili ya Elburgon DEB.
Glen alifariki papo hapo kutokana na majeraha ya risasi.
Wakazi wenye hasira walilaani utovu wa usalama katika eneo miezi michache baada ya kuuawa kwa Richard Otieno, na sasa wanataka haki kwa familia ya makanika huyo.
“Ni miezi miwili tu tangu tulipozika Richard Otieno na sasa tumepatwa na mauti mengine. Kinachokera ni kwamba aliuawa na mwili wake kutupwa nyuma ya kituo cha polisi. Nini kinafanyika Elburgon? Tunaelekea wapi?” James Kimani, mmoja wa mkazi, akauliza.
Baada ya mwanafunzi huyo kuuawa kwa kupigwa risasi, mwili wake ulitelekezwa kando ya barabara kwa saa kadhaa kabla ya polisi kuuchukua na kuupeleka katika Makafani ya Hospitali ya Kaunti Ndogo ya Molo.
Familia za mwanafunzi huyo na makanika waliouawa sasa wanataka uchunguzi wa haraka ufanywe ili wapate haki.
“Nilirauka kama kawaida na kuelekea shambani umbali wa kilomita kadhaa kutoka nyumbani. Mwendo wa saa nane na dakika 50 mchana nilipigiwa simu na mmoja wa marafiki zangu kwamba mwanangu amepigwa risasi katika maandamano. Mwanangu ameuawa na polisi kikatili na ninataka nitendewe haki,” akasema Bi Caroline Bitutu, mamake mwanafunzi huyo.