Siendi kwa Ruto, Gideon Moi sasa azungumza
MWENYEKITI wa KANU Gideon Moi amepuuzilia mbali miito kutoka kwa viongozi wa Kaunti ya Baringo kwamba aridhiane kisiasa na Rais William Ruto.
Wabunge wa eneo hilo wamekuwa wakimsihi Seneta huyo wa zamani wa Baringo afanye kazi na Dkt Ruto kwa ajili ya kukuza na kudumisha umoja wa kisiasa katika jamii ya Wakalenjin.
Gideon alikataa wito huo wikendi alipohutubu wakati wa ibada ya mazishi ya mbunge wa zamani wa Baringo Kaskazini Willy Kamuren katika Shule ya Msingi ya Ayiebo.
“Kuna taratibu nyingine zinazoendelezwa na zitakapokamilishwa nitarejea kwa wananchi kupata ushauri wao. Sihitaji handisheki na mtu yeyote isipokuwa na watu wa Baringo ambao ndio watanipa mwelekeo,” akasema Bw Gideon .
“Sihitaji handisheki, ninawahitaji nyie watu wetu. Wakati ukitimia, nitarejea kwenu ili mnionyeshe mkondo wa kufuata,” Bw Gideon akaongeza.
Seneta huyo wa zamani wa Baringo alisema hayo baada ya wabunge wa eneo hilo kudai kuwa Mbunge wa Tiaty William Kamket alijiunga na Kenya Kwanza kufanya maandalizi kwa kiongozi wa chama chake, Kanu, kujiunga na muungano huo tawala.
Bw Kamket aligura Azimio la Umoja-One Kenya baada ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi mkuu wa 2022.
Mbunge, huyo aliyetetea kiti chake kwa tiketi ya Kanu, alipokewa na Rais Ruto katika makazi rasmi ya Naibu Rais mtaani Karen, mnamo Septemba 1.
Bw Kamket ndiye alikuwa mbunge wa kipekee katika Kaunti ya Baringo aliyechaguliwa kwa tiketi ya chama tanzu cha Azimio. Eneo hilo ni ngome ya chama cha United Democratic Alliance (UDA).
“Nilipojiunga na Kenya Kwanza mnamo 2022, ni kama nilienda kukuandalia wewe (Moi) nafasi ya kujiunga na mregno huo, sasa wakati umefika kwako kujiunga na Kenya Kwanza ili tutembee pamoja,” Bw Kamket akasema.
“Nimekuwa humo kwa miaka miwili na nusu na ningetaka kukuhakikishia kuwa nyumba hiyo ni safi wala hamna miiba au hatari yoyote. Unavyoona niko sawa na nimeongeza uzani naomba uje ujiunge na serikali,” Mbunge huyo akaongeza.
Bw Kamket alisema aliwania kiti cha ubunge wa Tiaty kwa tiketi ya Kanu, lakini matokeo ya urais yalionyesha kuwa Rais Ruto kutoka jamii ya Wakalenjin ndiye alishinda.
Kwa hivyo, akaeleza, ilikuwa jambo la busara kwamba kujitokeza na kuunga mkono utawala wa sasa.
“Ilinibidi kusikiza sauti ya wapiga kura waliopigia kura Rais Ruto kwa kauli moja,” akasema Bw Kamket.
Kwa upande wake Mbunge wa Eldama Ravine Musa Sirma alisema ikiwa kiongozi wa Azimio Raila Odinga sasa anafanyakazi na Dkt Ruto aliyekuwa mpinzani wake mkuu, Bw Moi hana budi kufuata nyayo zake kwa kufanya handisheki na kiongozi wa taifa.
Lakini Bw Moi alimjibu hivi: “Kwa kuwa ningali na ninaelewana na wananchi, sihitaji kufanya handisheki na yeyote. Handisheki ninayohitaji ni ya watu wa Baringo pekee.”
Bw Moi alichelea kutangaza waziwazi ikiwa atawania kiti cha useneta wa Baringo kilichosalia wazi kufuatia kifo cha William Cheptumo.
Uchaguzi mdogo wa kujazi nafasi hiyo ni miongoni mwa chaguzi 14 zitakazofanyika mwezi Juni mwaka huu baada ya kuteuliwa kwa mwenyekiti mpya na makamishna sita wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).
Bw Moi alidai kuwa hajawahi kumtusi mtu yeyote na nia yake kuu ni kuhudumia wananchi na kuachana na siasa za mbaya.
Seneta huyo wa zamani wa Baringo alibwagwa na marehemu Cheptumo wa chama cha UDA katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022.
Alitetea kiti hicho, ambacho alikuwa amekishikilia kwa mihula miwili, kwa tiketi ya chama chake, Kanu, chini ya muungano wa Azimio.
Baadhi ya wakazi wa Baringo na viongozi wa kisiasa, wafuasi wa Bw Moi, sasa wanamtaka arejee ulingoni kuwania kiti hicho katika uchaguzi mdogo ujao.