Magaidi walivyokusanya wanakijiji, kuwahubiria na kuwagawia tende kabla ya kutoweka
MSAKO mkali umeanzishwa dhidi ya washukiwa karibu 150 wa ugaidi waliovamia kijiji cha Mangai kilicho katika msito wa Boni, Kaunti ya Lamu, ambapo walihubiri kabla kutoweka Jumamosi.
Akithibitisha uvamizi huo, Kamishna wa Kaunti ya Lamu Wesley Koech, alisema magaidi hao waliokuwa na silaha, ikiwemo bunduki, waliwakusanya wanakijiji mahali pamoja na kisha kuwahubiria mafundisho ya itikadi kali kwa dakika kadhaa kabla ya kuwagawia tende.
Baadayae, walitokomea ndani ya msitu wa Boni bila kuua wala kumjeruhi yeyote. Tukio hilo lilifanyika Jumamosi usiku.
Bw Koech hata hivyo aliwahakikishia raia usalama wao, akisema maafisa wa kutosha wa jeshi (KDF) na vitengo mbalimbali vya polisi tayari wako Mangai na viunga vyake kuwasaka magaidi hao.
Aliwasihi wananchi kushirikiana na walinda usalama na kuwa tayari kutoa ripoti zitakazosaidia kuwanasa wahalifu hao.
“Tuko imara kuona kwamba ndugu zetu Waislamu wanaadhimisha Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan bila kutatizwa. Kuna wahalifu ambao nia yao ni kutumia kipindi hiki cha Ramadhan kutatiza usalama wakitumia masuala ya dini.
“Sisi tunajua waliovamia Mangai Jumamosi, hata wakigawia waumini tende, wao bado ni magaidi na tutapambana nao. Wananchi wasiwe na shaka. Tushirikiane kuwakabili hao wahalifu,” akasema Bw Koech.
Baadhi ya wakazi wa Mangai waliohojiwa na Taifa Leo walisema kisa hicho kilitokea mwendo wa saa kumi na mbili unusu jioni.
Bw Gubo Salim, alieleza alikuwa ameketi mbele ya nyumba yake wakati ghafla alipoona kundi kubwa la watu wakiingia kijijini.
Kulingana na Bw Gubo, wengi walikuwa wamevalia sare zinazofanana na za kijeshi, jambo lililomfanya kutoshtuka akijua wao ni walinda usalama ambao kila siku hutekeleza doria na kuwalinda msituni Boni.

“Walipoingia kijijini kwetu, walijitambulisha kuwa wao ni Al-Shabaab. Kisha walitukusanya mahali pamoja na kutuhubiria kuhusu umuhimu wa kutii mafundisho ya dini ya Kiislamu na kuitetea kivyovyote vile. Walihubiri kwa karibu dakika thelathini.
“Baada ya mahubiri wakatugawia tende na kusisitiza kuwa wao si watu wabaya. Eti ni marafiki zetu. Kisha walitokomea msituni huku wakituonya kutofahamisha walinda usalama kuhusu ziara yao kijijini,” akasema Bw Gubo.
Mkazi mwingine wa Mangai waliyeomba kutotajwa jina alisema magaidi hao waliwaambia wao hawana tatizo na yeyote isipokuwa vikosi vya walinda usalama vya Kenya ambavyo vimekuwa vikitekeleza mauaji ya Waislamu wenzao ambao hawana hatia,” akasema mkazi huyo.
Si mara ya kwanza kwa magaidi wa Al-Shabaab kuvamia vijiji vya msitu wa Boni na kuhubiria wakazi.
Mnamo Agosti 2015, zaidi ya Al-Shabaab 100 walivamia kijiji cha Basuba kilichoko karibu kilomita 19 kutoka Mangai, ambapo waliwahubiria wananchi kwa zaidi ya saa moja.
Katika mwaka wa 2018, zaidi ya Al-Shabaab 50 waliojihami kwa silaha hatari walivamia kijiji cha Ishakani kilichoko mpakani mwa Kenya na Somalia, ambapo pia waliwahubiria wakazi kwa karibu saa moja. Mavamizi yote yalitekelezwa maji