Habari za Kitaifa

Serikali yashindwa kumtetea Adamson Bungei kufuatia maafa ya Gen Z wakati wa maandamano

Na JOSEPH WANGUI March 18th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WAKUU wa polisi sasa watawajibikia mauaji ya waandamanaji waliopinga Mswada wa Fedha wa 2024, yaliyotekelezwa na maafisa wa usalama, baada ya kesi iliyolenga kuwakinga kutupiliwa mbali.

Mahakama Kuu ilizima pingamizi kutoka kwa serikali kuhusu kesi hiyo pamoja na pendekezo la kutaka mzozo huo ushughulikiwe na Kitengo cha Kuadhibu Maafisa Watundu katika Huduma ya Kitaifa ya Polisi (IPU) na Mamlaka ya Kufuatilia Utendakazi wa Polisi (IPOA).

Chama cha Mawakili Nchini (LSK) kiliwasilisha kesi dhidi ya aliyekuwa Kamanda wa Polisi Nairobi Adamson Bungei na aliyekuwa Afisa Msimamizi wa Kituo cha Polisi cha Central Moses Mutayi kwa “ukiukaji sheria” wakati polisi walipokabiliana na waandamanaji mnamo Juni 2024.

Chama hicho pia kilisema kuwa wakuu hao wawili wa polisi wanapaswa kuadhibiwa kutokana na visa vya kudhulumiwa kwa mawakili wakati wa maandamano hayo.

Kesi hiyo pia inahusu kuuawa kwa waandamanaji wawili, Rex Masai na mwanaume aliyetambuliwa kama Evan, aliyeuawa kwa kupigwa risasi na polisi Juni 18, 2024 katikati mwa jiji la Nairobi.

Pia, inahusisha kudhulumiwa na kutishwa kwa mawakili, walioingilia kati kutetea vijana waliokamatwa na maafisa wa polisi.

LSK, kulingana na stakabadhi ilizowasilisha kortini, inasema kuwa Bw Bungei na Bw Mutayi “waliwaagiza maafisa wao kuwarushia mawakili na waandamanaji vitoza machozi na risasi halisi na silaha zingine hatari.”

Waandamanaji hao walikuwa wakipinga mapendekezo kwenye Mswada wa Fedha 2024 ya kuongezwa kwa ushuru.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Inspekta Jenerali Mkuu wa Polisi, tume ya NPS na Mwanasheria Mkuu.

Walishtakiwa kwa madai ya kufeli “kuzuia utekelezaji wa vitendo vinavyokiuka sheria” na polisi wanapopambana na waandamanaji.

Ikijibu na kupinga kesi hiyo, serikali iliitaja kama isiyofaa.

Iliitaka mahakama kutupilia mbali kesi hiyo kwa sababu inaibua masuala ambayo yangeshughulikiwa na kitengo cha kuwaadhibu polisi watundu (IPU) au mamlaka ya IPOA.

Kupitia Wakili Mkuu wa Serikali Samuel Kaumba, washtakiwa walisema LSK ingewasilisha malalamishi yao kwa asasi hizo inavyohitajika na Sheria ya Huduma ya Kitaifa ya Polisi kabla ya kuelekea kortini.