Idara yatabiri mvua itanyesha sehemu nyingi siku saba zijazo
IDARA ya Hali ya Hewa ya Kenya imetabiri kuwa mvua itaendelea kunyesha katika sehemu nyingi za nchi kwa siku saba zijazo, huku baadhi ya maeneo, ikiwemo Nairobi, yakitarajiwa kushuhudia mvua kubwa.
Katika utabiri uliochapishwa Jumatatu unaohusu Jumanne, Machi 18, hadi Jumatatu, Machi 24, idara hiyo imetabiri mvua asubuhi katika sehemu za Nyanda za Juu Mashariki mwa Bonde la Ufa (ikiwemo Kaunti ya Nairobi), pamoja na manyunyu wakati wa usiku katika baadhi ya maeneo.
Sehemu hii, inayojumuisha kaunti za Nyandarua, Laikipia, Nyeri, Kirinyaga, Murang’a, Kiambu, Meru, Embu, Tharaka-Nithi, na Nairobi, inatarajiwa kuwa na mvua asubuhi katika maeneo machache.
Kwa mujibu wa Idara ya Hali ya Hewa, mvua inatarajiwa kusambaa katika maeneo kadhaa hasa katika nusu ya kwanza ya kipindi cha utabiri, kuanzia Jumanne hadi Alhamisi.
“Manyunyu ya mchana na radi zinatarajiwa kutokea maeneo mengi katika nusu ya kwanza ya kipindi cha utabiri, kisha kupungua katika sehemu chache baadaye,” idara hiyo ikaeleza.
Nyanda za Juu Magharibi mwa Bonde la Ufa, Ukanda wa Ziwa Victoria, na Bonde la Ufa – kaunti za Nandi, Kakamega, Vihiga, Bungoma, Siaya, Busia, Baringo, Nakuru, Trans-Nzoia, Uasin-Gishu, Elgeyo-Marakwet, West-Pokot, Kisii, Nyamira, Kericho, Bomet, Kisumu, Homabay, Migori, na Narok —zinatarajiwa pia kushuhudia mvua kwa siku saba.
Utabiri unaonyesha kuwa maeneo ya nyanda za chini za kusini-mashariki-kaunti za Machakos, Kitui, Makueni, Kajiado, na Taita-Taveta – pamoja na sehemu za bara za Kaunti ya Tana River, zitashuhudia mvua asubuhi, mchana, na usiku.
Kwa mujibu wa idara hiyo, radi zinatarajiwa katika baadhi ya maeneo.
Katika kaunti za Mombasa, Kilifi, Lamu, na Kwale, mvua inatarajiwa kuendelea mchana kutwa, huku manyunyu yakitarajiwa asubuhi, alasiri, na usiku.
Kaunti za Marsabit, Mandera, Wajir, Garissa, na Isiolo zinapaswa kujiandaa kwa mvua za asubuhi, pamoja na manyunyu na radi nyakati za alasiri na usiku kati ya Jumanne na Ijumaa.