Kaunti zinavyofyonza mali ya umma
KAUNTI kadhaa zilitumia mamilioni ya pesa kugharamia safari hewa za ndani na nje huku katika kaunti moja, afisa akisajili na kutumia nambari ya simu ya mkono kukusanya ushuru.
Katika miradi mikubwa ya ujenzi, ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Nancy Gathungu, imeonyesha mwelekeo ambapo baadhi ya wanakandarasi walitumia vifaa duni baada ya kutia mfukoni mamilioni ya pesa kwa kushirikiana na maafisa wa kaunti.
Ripoti hiyo pia ilionyesha kuwa kaunti zilitumia mamilioni ya pesa kwa mafunzo na kongamano hewa.
Katika kaunti ya Kericho, ukaguzi ulifichua zaidi jinsi afisa mmoja alisajili na kutumia nambari ya simu ya mkono ambayo haikuidhinishwa na hazina ya kaunti kukusanya ushuru.
“Taarifa za nambari hiyo zilionyesha mkopo wa Sh152, 290 na zingine Sh141, 852 kwa kipindi cha kuanzia Januari 24, 2024 hadi Agosti 5, 2024,” inasema ripoti hiyo.
Uchunguzi wa ndani kuhusu suala hilo ulipendekeza afisa huyo achukuliwe hatua kisheria.
Afisa mkuu wa kaunti chini ya Gavana Eric Mutai pia anamulikwa kwa kulipa watu binafsi Sh5, 786, 604 kwa safari za ndani na za nje.
Aidha, mapitio ya taarifa za benki za maendeleo na maelezo ya malipo ya IFMIS yalibaini malipo kwa watumishi mbalimbali ya Sh10, 683, 750 kwa safari za ndani na za nje na yote yalifanywa bila kuidhinishwa.
Ripoti hiyo pia inaonyesha ukiukaji mkubwa hasa katika ujenzi wa miradi.
Iliyojumuishwa katika miradi hiyo kuu ni mapendekezo ya ujenzi wa chumba cha upasuaji katika hospitali ya Kaunti Ndogo ya Ainamoi, iliyokadiriwa kuwa Sh14, 135, 859 na tarehe ya kukamilika Juni 4, 2020.
Muda wa kandarasi uliongezwa hadi Agosti 19, 2022.
“Mradi ulikuwa na bajeti iliyotengewa Sh12, 900, 000. Hata hivyo, ukaguzi wa eneo hilo Septemba 2024 ulibaini kuwa mradi ulikuwa umekwama.”
Katika kaunti ya Vihiga, usimamizi wa Gavana Wilber Ottichilo unamulikwa kuhusu matumizi ya Sh94 milioni kwa ajili ya ujenzi wa mochari ya kisasa katika Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Vihiga.
Uhakiki wa rekodi za mradi ulibaini kuwa kandarasi hiyo ilitiwa saini Februari 2021 kwa gharama ya Sh96.6 milioni kwa muda wa mwaka mmoja.
Hata hivyo, mnamo Julai 2022, aliyekuwa akishughulika na mradi huo aliomba nyongeza ya pesa ambayo iliidhinishwa.
Katika Kaunti ya Busia, afisa mkuu wa kaunti hakuweza kueleza jinsi Sh16 milioni zilizotumiwa kwa marupurupu ya kila siku.