Akili MaliMakala

Kahawa maalum kuwahi masoko bora

Na SAMMY WAWERU March 19th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KAHAWA ya Kenya imeorodheshwa miongoni mwa zile bora zaidi ulimwenguni, hii ikiwa ni kutokana na ladha yake ya kipekee. 

Zaidi ya asilimia 90 ya kahawa inayozalishwa nchini, inauzwa ng’ambo.

Masoko ya Bara Uropa yanachukua karibu asilimia 60 ya bidhaa hii.

Kulingana na New KPCU, chama cha muungano wa ushirika kusaga kahawa na kuitafutia soko, masoko mapya kama vile Japan na Korea yameanza kumezea mate kahawa ya Kenya.

Chama hicho ni kati ya mashirika ya serikali kuboresha sekta ya kahawa.

Washirika kwenye mtandao wa kiungo hiki cha kinywaji, wanaendelea kufanya bidhaa hii kuwa na ushindani mkuu kisoko.

Maharagwe ya kahawa yaliyochomwa tayari kusagwa. PICHA|SAMMY WAWERU

Coffeebee Processors Ltd, ni mojawapo ya kampuni zinazoongeza kahawa thamani kwa kuisindika.

Ikiwa na kiwanda chake eneo la Syokimau, Nairobi, kampuni hii huunda kahawa maalum.

Kwa Kiingereza, kahawa hii ya kipekee inajulikana kama specialty coffee. 

“Ni kahawa ya hadhi ya juu (daraja la kwanza), ambayo sokoni hushindaniwa mithili ya mahamri moto,” anasema Silas Majani kutoka Coffeebee Processors Ltd.

Kwenye Makala ya 19 ya Maonyesho ya Kahawa, yaliyofanyika Februari 13 na 14 katika Taasisi ya Utafiti wa Kahawa Nchini, Ruiru, ndiyo Coffee Research Institute (CRI), kampuni hiyo ilivutia watu kutokana na kahawa yake ya upekee.

Kazuri na Coffeebee Instant, ni brandi ambazo Coffeebee Processors Ltd huunda.

Mbuni za kahawa. PICHA|SAMMY WAWERU

“Ni kahawa yenye ladha tamu, ambayo inadumisha hadhi ya kahawa ya Kenya – dhahabu nyeusi,” Majani akaambia Akilimali kwenye mahojiano ya kipekee Maonyeshoni.

Dhahabu nyeusi, ni jina la majazi la kahawa kutokana na thamani yake kubwa.

Kampuni hiyo pia inashiriki katika uzalishaji wa kahawa (maharagwe ya kahawa), Majani akifichua kwamba ina zaidi ya ekari 1, 000 Nyeri – mojawapo ya kaunti zinazoongoza katika uzalishaji wa kahawa nchini.

“Pia, tuna kandarasi na wakulima ambao hutusambazia maharagwe ya kahawa,” akadokeza.

Afisa kutoka New KPCU akielezea kuhusu soko la kahawa maalum. PICHA|SAMMY WAWERU

Kuendeleza mdahalo wa kuvutia wanywaji wa kahawa nchini, kwenye maonyesho hayo ya Ruiru ambayo kauli mbiu yake ilikuwa ‘Advancing agricultural innovation for resilient food systems and sustainable livelihoods’, Coffeebee Processors Ltd ilitumia jukwaa hilo kuandalia waliofika kahawa.

“Ndio maana tulibeba ‘mashine’ za kupika kahawa,” Majani akasema.

Kando na kuteka masoko ya ndani kwa ndani, kampuni hiyo pia huuza bidhaa zake nje ya nchi, katika mataifa kama Uturuki na Amerika.

Kulingana na data za Mamlaka ya Chakula na Kilimo Nchini (AFA), inakadiriwa kahawa inakuzwa kwenye Hekta 114,000, hii ikiwa ni ongezeko kutoka Hekta 109,000 miaka michache iliyopita.

Kiwango cha uzalishaji kahawa kinachezea Tani Metri (MT) 38,000 hadi 50,000MT kwa mwaka.

Gredi MH na ML ya kahawa. PICHA|SAMMY WAWERU

Mwaka 1987, ndio Kenya ilivunja historia kwa kuzalisha zaidi ya 127,000MT, kiwango ambacho Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Kahawa (CRI), Dkt Elijah Gichuru anaamini kinaweza kurejelewa endapo kila mkahawa utazalisha kati ya kilo nane hadi kumi.

“Hata ingawa kuna wakulima ambao huandikisha kuvuna kilo 30 hadi 40 kwa mti kwa mwaka, japo ni nadra sana, tukifanya bidii kila mkahawa uzae wastani wa kilo 10 kwa mwaka, tutawahi rekodi ya 1987,” anaelezea Dkt Elijah Gichuru.

CRI ni kati ya taasisi 17 zinazohudumu chini ya Shirika la Utafiti wa Kilimo na Mifugo Kenya (KALRO).

Taasisi hiyo inajukumika kutafiti kuhusu masuala ya kahawa na kutoa mwelekeo.

Wakulima wakielimishwa kuhusu kahawa wakati wa Maonyesho ya Kahawa 2025 katika taasisi ya utafiti wa kahawa KALRO, Ruiru. PICHA|SAMMY WAWERU