Akili MaliMakala

Himizo wakulima wazingatie jenetiki za nguruwe kufanikisha ufugaji

Na SAMMY WAWERU March 20th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

KANDO na kuzingatia ubora wa chakula, matibabu na mazingira ya nguruwe, jenetiki (genetics) ni kigezo muhimu kufanikisha ufugaji wa wanyama hawa wa nyumbani.

Miaka ya hivi karibuni, ufugaji wa nguruwe umeonekana kukumbatiwa na wafugaji wengi kufuatia urahisi wake kulea.

Ongezeko la kiwango cha buchari, hususan maeneo ya mijini, ni ishara ya sekta kukua.

Huku wakulima wakishabikia ufugaji nguruwe, wataalamu wanahimiza haja ya kuzingatia jenetiki.

Dkt Godfrey Wamai, msimamizi wa mifugo katika Kampuni ya Farmers Choice Ltd. PICHA|SAMMY WAWERU

Dkt Godfrey Wamai, msimamizi wa mifugo katika Kampuni ya Farmers Choice, anasisitiza umuhimu wa jenetiki kufanikisha ufugaji wa nguruwe.

Farmers Choice Ltd, ni kampuni tajika katika usambazaji wa nyama za nguruwe, kuongeza thamani na ufugaji.

“Jenetiki ni muhimu sana. Ikiwa mnyama ana jenetiki nzuri, kiwango chake cha ubadilishaji wa chakula kuwa nyama ni cha juu,” anasema Dkt Wamai.

Farmers Choice imekumbatia teknolojia ya kisasa, Artificial Insemination (AI) kutungisha nguruwe ujauzito.

Dkt Godfrey Wamai, msimamizi wa mifugo katika Kampuni ya Farmers Choice akielezea kuhusu umuhimu wa jenetiki. PICHA|SAMMY WAWERU

Mfumo huu wa Uhamilishaji kwa lugha ya Kiswahili, Dkt Wamai anasema unafanikisha kupata mifugo wenye ubora wa juu, hivyo basi kupata bridi zinazohimili mikumbo ya athari za mabadiliko ya tabianchi.

Farmers Choice inaendesha kituo maalum cha kuzalisha, kufuga nguruwe, kutengeneza chakula cha nguruwe, na kuzalisha nyama, kinachojulikana kama Rosemark, kilichopo Limuru, Kaunti ya Kiambu.

Kituo hicho, vilevile hutoa mafunzo bora ya ufugaji nguruwe na pia kuwa na mikataba na wakulima.

Wakulima wakifunzwa kuhusu jenetiki za nguruwe. PICHA|SAMMY WAWERU

Laban Kabiru, Meneja Mkuu Farmers Choice, anasema huwapa wakulima mifugo inayokua haraka na kuzalisha kiwango cha juu cha nyama.

‘Tunatoa mafunzo ya ana kwa ana, pia kupitia mitandao ya kijamii kwa wakulima kote nchini kuhusu mbinu bora za ufugaji nguruwe, ikiwa ni pamoja na mwongozo wa kuchagua mifugo bora,” Kabiru anaelezea.

Laban Kabiru, Meneja Mkuu Farmers Choice, wakati wa mahojiano. PICHA|SAMMY WAWERU

Kulingana na afisa huyu, kampuni hiyo inazingatia aina tatu za nguruwe, ambazo ni; Large White, Landrace, na Duroc.

Mbegu za spishi hizo, huchanganywa kupitia ujamiishaji ili kupata bridi bora.

Kituo chake cha ufugaji nguruwe, Rosemark, pia husambaza mbegu za AI kwa wakulima.

Wakulima wakifuatilia mafunzo ya ufugaji wa nguruwe yaliyofanywa majuzi na Farmers Choice. PICHA|SAMMY WAWERU