Rubiales akwepa jela, atozwa faini ya Sh1.4 bilioni kwa kubusu mwanasoka kwa lazima
ALIYEKUWA mkuu wa kandanda nchini Uhispania, Luis Rubiales, 47, amepatikana na hatia ya kumbusu mwanasoka Jenni Hermoso bila idhini baada ya fainali ya Kombe la Dunia la Wanawake mnamo 2023.
Bosi huyo wa zamani wa Shirikisho la Soka la Uhispania (RFEF), ameponea kufungwa jela baada ya kuamriwa kulipa faini ya zaidi ya Sh1.4 milioni ili kumaliza kashfa hiyo ya “Kissgate”.
Mahakama Kuu ya Uhispania ilimhukumu Rubiales kwa hatia ya unyanyasaji wa kingono wakati wa fainali ya Kombe la Dunia 2023 jijini Sydney, Australia, ambapo Uhispania iliishinda Uingereza 1-0 kupitia kwa bao la Olga Carmona.
Mahakama ilimpiga Rubiales faini ya zaidi ya Sh1.4 milioni na kumwachilia huru pamoja na washtakiwa wengine watatu katika kesi hiyo kuhusu busu la kulazimisha. Waendeshaji mashtaka walikuwa wameomba korti ipokeze Rubiales hukumu ya kifungo cha miaka miwili na nusu gerezani.
Rubiales amekanusha mara kwa mara makosa yote aliyoshtakiwa kwayo, akisisitiza busu lake kwa Hermoso lilikuwa “ishara ya mapenzi kati ya marafiki waliozoeana walipokuwa wakisherehekea ushindi” na wanaomshutumu ni watu “wenye wivu na nia mbaya.”
Taarifa kutoka kwa mahakama ilisema: “Uamuzi unataka Rubiales kutowahi kumkaribia Hermoso kwa mita 200 na kutowasiliana naye kabisa ndani ya kipindi cha mwaka mmoja.”
Mapema mwezi huu, Hermoso, 34, alifika katika Mahakama ya Audiencia Nacional jijini Madrid na akaeleza jinsi Rubiales alivyomshika kichwa kwa nguvu kumbusu bila ridhaa yake.
Aliambia korti kuwa busu hilo la kulazimishiwa kutoka kwa Rubiales, “lilichafua moja kati ya siku alizostahili kuzifurahia zaidi maishani”.
“Nilishtukia nimeshikwa kichwani kwa lazima huku nikipigwa busu midomoni. Nilihisi haikuwa sawa kabisa. Sikutarajia kitu kama hicho kutoka kwa bosi wangu na tena kitokee katika mazingira yale. Busu la midomoni hutolewa tu ninapoamua kufanya hivyo.”
Aliongeza: “Kama mwanamke, nilihisi kukosewa heshima. Ni tukio moja lililoharibu mojawapo ya siku nilizostahili kuzifurahia zaidi maishani. Shinikizo za kuacha baadaye kufuatilia haki na hofu ya usalama wangu ilinilazimisha kuhama Madrid.”
“Pindi niliporejea Uhispania baada ya Kombe la Dunia, kamera zilikuwa zikinifuata kila mahali usiku na mchana. Nilipigwa picha na kurekodiwa na kila mtu, hata nikishiriki mlo na familia yangu. Ilinibidi kuondoka Madrid pamoja na familia yangu. Nilitishiwa maisha na ikabidi tuondoke sote Madrid. Maisha yangu yalibadilika kabisa kutoka siku hiyo.”
Mahakama pia iliambiwa kuwa saa chache baada ya busu hilo, Rubiales na wasaidizi wake walianza kumshinikiza Hermoso atangaze kuwa ni kitu kilichofanyika kwa ridhaa yake. Aliondolewa kwenye basi la timu jijini Sydney na kuonyeshwa taarifa ya ‘uongo’ ambayo alitarajiwa kutia sahihi akiungama kuwa yeye na Rubiales ni wapenzi wa dhati waliopanga kufunga pingu za maisha.
Hatimaye Rubiales alijiuzulu mnamo Septemba 2023 kufuatia msukosuko uliosababishwa na kashfa hiyo. Alipigwa marufuku ya kutojihusisha na masuala ya soka kwa miaka mitatu mnamo Oktoba 2023 kutokana na mienendo yake katika fainali hiyo ya Kombe la Dunia jijini Sydney.