Habari za Kitaifa

Mashirika yazindua mkakati kupiga vita ufisadi

Na NDUBI MOTURI March 26th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MASHIRIKA ya Serikali yameahidi kushirikiana katika kupambana na ufisadi unaozuia upatikanaji wa haki nchini kwa kutumia mbinu ya pamoja.

Katika uzinduzi wa mkakati wa kupambana na ufisadi katika sekta ya haki jijini Nairobi, Idara ya Mahakama imesema itaimarisha uwezo wake kupitia mafunzo ya mara kwa mara kwa maafisa wake na kuanzisha nambari ya simu bila malipo ambapo Wakenya wataweza kuripoti wale wanaoitisha hongo mahakamani.

Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) ameahidi kuharakisha kesi za uhalifu wa kiuchumi na kuhakikisha kuwa wanaoiba mali ya umma wanakabiliwa na mkono wa sheria ili mali iliyoibwa irejeshwe.

Hazina ya Taifa pia imesema itahakikisha kuwa fedha zinapatikana kwa mashirika ya serikali yanayopambana na ufisadi ili kuhakikisha haki inatendeka na kuzuia wizi wa mali ya umma.

Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) imeeleza kuwa imejitolea kutumia hatua za kuzuia, ufuatiliaji na urejeshaji wa mali ili kuimarisha vita dhidi ya ufisadi.

Jaji Mkuu Martha Koome, ambaye ni mwenyekiti wa Baraza la Kitaifa la Usimamizi wa Haki (NCAJ), amesema kuwa mbinu ya pamoja katika kupambana na ufisadi itasaidia serikali kupunguza kupotea kwa rasilimali na kuhakikisha huduma zinafikia wananchi.

DPP Renson Ingonga ametoa wito kwa mashirika ya serikali kushirikiana kwa karibu zaidi kupambana na ufisadi. “Tumepata hukumu dhidi ya magavana wa zamani Ferdinand Waititu na Daniel Waithaka, lakini kesi hizi huchukua hadi miaka mitano. Tunahitaji mikakati ya uchunguzi wa haraka, mashtaka na uamuzi ili kuhakikisha haki inatendeka,” alisema.

Waziri wa Hazina ya Taifa, John Mbadi, amesema kuwa ufisadi unaathiri uchumi wa nchi na kuahidi kuwa serikali itahakikisha mashirika yote yanayopambana na ufisadi, ikiwemo mahakama, yanapata ufadhili wa kutosha.

Inspekta Jenerali wa Polisi, Douglas Kanja, amesema wanashirikiana na EACC kubaini mianya ya ufisadi ndani ya polisi na kuiziba.

Rais wa Chama cha Wanasheria Kenya (LSK), Faith Odhiambo, amesema ufisadi ni tishio kwa utekelezaji wa haki za binadamu kama zilivyoainishwa katika Katiba na kuwataka wadau wote kushirikiana katika kupambana nao.

Mikakati iliyozinduliwa inalenga maeneo manne makuu: kuimarisha uratibu wa mashirika ya haki, kuboresha mazingira ya kisheria na kiutawala, kuharakisha kesi za ufisadi, na kutumia teknolojia kuzuia mianya ya ufisadi.

Kwa mbinu hizi, sekta ya haki inatarajia kuimarisha vita dhidi ya ufisadi na kuhakikisha haki inapatikana kwa wote.