Maoni: Serikali ya Ruto inapalilia ufisadi kutoa barua za ajira kwa wanasiasa waipigie debe
HABARI kwamba wanasiasa wanaounga serikali wanakabidhiwa nafasi za ajira ili kunufaisha watu wanaopenda kuipigia debe utawala wa sasa ni ufisadi wa hali ya juu.
Kwa hakika hatua hii inaonyesha jinsi maadili yetu yameoza na jinsi serikali inavyoendesha ufisadi na ubaguzi katika uajiri.
Ni ukiukaji wa haki, usawa na kanuni za uajiri za serikali na kutwaa majukumu ya idara na tume za serikali ambazo zinasimamia ajira ya watumishi wa umma.
Labda hii ndio sababu kuna mswada unaopendekeza Tume ya Utumishi wa Umma ipokonywe mamlaka ya kuajiri na kuhamisha watumishi wa umma yatwikwe Mkuu wa Utumishi wa Umma.
Bila mabadiliko ya sheria, tume kama ya huduma ya walimu (TSC) ambayo wanasiasa wamekuwa wakitoa barua za ajira katika mikutano ya hadhara inapaswa kueleza kwa nini inatoa majukumu yake kwa watu wengine kwa sababu ndiyo imejukumiwa uajiri wa walimu.
Iwapo nafasi za ajira zinatolewa na wanasiasa au wawe ndio wa kuamua anayefaa kuajiriwa, inamaanisha kuwa watu waliohitimu na wasio na ushawishi wa kisiasa hawataweza kupata ajira na pia utendakazi wa watu wanaokabidhiwa barua hizi mitaani unaweza kuwa wa kutiliwa shaka kwa kuwa uwezo wao hautathminiwa na uaminifu wao utakuwa kwa wanasiasa na wala sio kwa mwajiri wao ambaye ni tume.
Yote tisa, kumi ni kuwa kinachoendelezwa na wanasiasa na kwa kiwango kikubwa na serikali inayosemekana kuwapa barua hizi wagawe au wauzie watu, ni ufisadi ambao imekuwa ikiahidi kuangamiza.
Hakuna njia ambayo serikali itaweza kupiga vita uovu ambao inaupalilia na hivyo basi inachofanya ni kukita ufisadi sio tu serikalini, bali pia katika jamii.
Matokeo yake ni kuendeleza ubaguzi ambao pia inadai kukumbatia.