Michezo

Mke wa Onana ajua hajui baada ya kuporwa Uingereza

Na MWANDISHI WETU April 7th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MELANIE Kamayou ambaye ni mke wa golikipa wa Manchester United, Andre Onana, ndiye wa hivi karibuni kujipata pabaya mikononi mwa wezi sugu wa eneo la Cheshire huko Uingereza baada ya kupokonywa saa aina ya Rolex na begi la Hermes Birkin lenye thamani ya Sh10.4 milioni.

Mwanamitindo huyo aliporwa mamilioni ya pesa na kunyang’anywa vitu hivyo vya thamani nje ya mkahawa wa Kiitaliano huko Cheshire mnamo Machi 29, 2025.

Liam Ross, 25, kutoka eneo la Wibsey huko Bradford, ameshtakiwa kwa kutekeleza wizi huo, gazeti la ‘Daily Mail’ limeripoti.

Mwizi huyo alifikishwa katika Mahakama ya Chester Ijumaa iliyopita, akikabiliwa pia na shtaka jingine la kusambaza bangi.

Anatarajiwa kufikishwa tena katika Mahakama ya Chester mwanzoni mwa mwezi ujao.

Melanie, ambaye anajieleza mtandaoni kama mfamasia, mfanyabiashara na mfadhili wa miradi mbalimbali, mara nyingi hupakia picha na video akijinaki na baadhi ya mali zake za thamani kubwa.

Mojawapo ya bidhaa hizo ni begi lake la Hermes Birkin la Sh10.4 milioni.

Mkoba huo ni adimu sana na ni miongoni mwa ile inayotafutwa kwa wingi zaidi mitandaoni na wanawake matajiri ulimwenguni kote.

Mikoba ya Hermes Birkin imekuwa ikiuzwa na kununuliwa kwa mamilioni ya pesa huku ya bei ghali zaidi kuwahi kuuzwa ikigharimu Sh252 milioni.

Melanie ni miongoni mwa wanawake wachache sana duniani ambao ni wamiliki wa mikoba hiyo.

Kipusa huyo amekuwa akiishi na Onana katika ndoa tangu 2023 na wanaripotiwa kuwa na mtoto wa kiume pamoja.

Walihamia Uingereza wakati Onana aliposajiliwa na Man-United kutoka Inter Milan ya Italia Julai 2023.

Tangu wakati huo, amedakia miamba hao katika jumla ya mechi 93.

Wanandoa hao sasa wanaishi katika mtaa wa Alderley Edge, kivutio cha nyota wa sasa na wa zamani wa EPL.

Eneo hilo limepewa jina la utani “Knightsbridge of the North” na ni nyumbani kwa baadhi ya wanasoka tajika wanaomiliki magari ya thamani kubwa.

Cristiano Ronaldo, David Beckham, Rio Ferdinand, Wayne Rooney na Jordan Henderson pia wamewahi kuishi mahali hapo.

Trent Alaxander-Arnold, Raheem Sterling na Virgil van Dijk ni miongoni mwa wanasoka wa sasa wa EPL wanaoishi katika mtaa wa Alderley Edge kwa sasa.