Habari za Kitaifa

Spika wa zamani Kisii atiwa mbaroni wafuasi wake wakidai anawindwa kwa kuunga Matiang’i kuwa rais

Na WYCLIFFE NYABERI April 8th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

SPIKA wa zamani wa Bunge la Kaunti ya Kisii David Kombo na Naibu Karani David Omwoyo wamefikishwa mahakamani baada ya kukamatwa na makachero wa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC).

Wawili hao wanalaumiwa kwa matumizi mabaya ya afisi na kuajiri mtu kinyume cha sheria katika gatuzi hilo mtawalia.

Bw Kombo, ambaye amewahi kuhudumu kama Mbunge wa Mugirango Kusini kwa mihula miwili, alifikishwa mahakamani Jumanne, Aprili 7, 2025 huku Bw Omwoyo akiwasilishwa siku moja mapema.

Maelezo ya mashtaka ni kwamba Bw Omwoyo, kinyume na utaratibu na kinyume cha sheria alimteua mpwa wake, Bi Everline Maraburi kuwa karani katika Bunge la Kaunti, bila idhini ya Bodi ya Utumishi wa Umma ya Kaunti au kufuata taratibu zilizowekwa za kuajiri, miaka minane iliyopita.

EACC ilisema alipoteuliwa, Bi Maraburi alihudumu kama Msaidizi wa Kibinafsi wa Bw Kombo (PA) kwa mkataba wa kudumu kinyume na kanuni za Tume ya Mishahara na Marupurupu (SRC).

Huku Bw Kombo akiitikia kuajiriwa kwa Bi Maraburi, EACC ilisema alitumia ofisi yake vibaya.

Akiwa mbele ya Hakimu Mkuu Mwandamizi Joshua Nyariki, Bw Kombo alikana shtaka hilo.

Mapema kabla ya Bw Kombo kukana mashtaka, mawakili wake Wilkins Ochoki na George Morara waliomba mteja wao asijibu mashtaka hadi wiki ijayo.

Wawili hao waliteta kuwa mshtakiwa mwenza wa Bw Kombo alipowasilishwa kortini, mahakama ilitoa maagizo ya kumtaka afike kortini Aprili 14.

Pia, waliongeza kuwa Bw Kombo hawezi kutoroka kwa sababu ni mfanyabiashara maarufu mjini Kisii na pia kwa sababu matatizo ya kiafya.

“Mheshimiwa, mteja wetu alifanyiwa upasuaji wa moyo juzijuzi tu. Ana Kisukari, shinikizo la damu na maisha yake yatakuwa hatarini ikiwa ataendelea kuzuiliwa. Isitoshe, hayuko hatarini kutoroka na kwa hivyo tunaomba umwachilie bila dhamana yoyote,” Bw Ochoki aliomba.

Hata hivyo, Hakimu alimwachilia Bw Kombo kwa dhamana ya pesa taslimu Sh50,000 au bondi ya Sh100,000. Masharti sawia pia yalipewa Bw Omwoyo alipowasilishwa mahakamani.

Akihutubia wanahabari baada ya kikao cha mahakama, wakili wa Bw Kombo, George Morara alidai kukamatwa kwa spika huyo wa zamani kulichochewa kisiasa.

Hata hivyo, hakufichua walio nyuma ya masaibu ya mteja wake.

“Maafisa waliotekeleza kukamatwa kwa Bw Kombo jijini Nairobi walikuwa chini ya maelekezo na maagizo kutoka kwa mtu fulani. Ninaweza kuhusisha watu fulani au watu fulani lakini siwezi kubainisha wanaomuwinda,” Bw Morara alisema.

Wafuasi wengi wa Bw Kombo, waliomiminika kortini wakati wa kuwasilishwa kwake, walidai kuwa kukamatwa kwa spika huyo wa zamani Kisii kunahusiana na tangazo lake la hadharani kwamba anaunga mkono azma ya aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang’i kugombea urais 2027.

Wiki mbili zilizopita, Bw Kombo aliongoza kundi la wazee kutoka ukoo wake wa Abagirango, kutangaza hadharani kuwa wanaunga mkono azma ya Dkt Matiang’i.

“Tangu 2017, walikuwa wapi? Kwa nini wangoje kwa miaka minane. Hii ni njama ya kumnyamazisha tu,” Alloys Moseti alidai.