Demu ataka Palmer amfunge bao la mahaba haraka upesi
KICHUNA Connie Grace amemtaka mchumba wake Cole Palmer anayechezea Chelsea na timu ya taifa ya Uingereza kufanya hima na kumfunga bao kabambe la kimapenzi.
Grace alianika matamanio yake hayo wiki hii akiwa likizoni Montego Bay, Jamaica.
Palmer alianza kutikisa buyu la asali la Grace mwanzoni mwa mwaka jana, 2024, na wakavishana pete za uchumba mnamo Julai mwaka huo.
“Mwaka mmoja ushapinduka katika uhusiano wetu na penzi limekuwa spesheli. Namhimiza Palmer sasa afanye haraka upesi apachike wavuni bao la kufungua kazi,” akaandika mrembo huyo kwenye Instagram alikopakia baadaye picha kadhaa akiwa amejikwatua ndani ya bikini ya kijani kibichi huku akishikilia nazi mkononi.
Awali, kidosho huyo ambaye ni mtaalamu wa kurembesha kucha jijini Manchester alinaswa na kamera akisisimuana kimapenzi na Palmer katika mkahawa mmoja wa kifahari jijini London, Uingereza.Rafiki wa karibu wa kidosho huyo aliyehojiwa na gazeti la The Sun alisema: “Wote ni wachanga na ni marafiki wakubwa. Walifurahia pia majira ya joto pamoja walipokuwa likizoni huko Ibiza, Uhispania. Wanapendana sana na lengo lao ni kufunga pingu za maisha.”
Kwenye mojawapo ya picha ambazo Grace alibwagia zaidi ya mashabiki wake 35,000 Instagram, Palmer alikuwa akitabasamu huku akiwa amemkumbatia Connie ambaye kichwa chake kilikuwa kimetua juu ya bega la kushoto la dume lake.
Kwenye video nyingine, videge hao walionekana wakiwa wamejipumzisha nyuma ya boti katika ufuo wa Ibiza nchini Uhispania huku Palmer akitazama simu yake.
Baada ya kubadilishana kasia na kuchezea maji kwa kurushiana kwa mikono, walionekana wakirukia ndani ya mashua ya kifahari walikojianika kwa muda.
Walipigana pambaja baadaye kila mmoja akijilegeza kimapenzi kwa mwenzake.