Ishara tosha Ruto aliambulia pakavu ziara ya Mlima Kenya
ZIARA ya hivi majuzi ya Rais William Ruto katika eneo la Mlima Kenya iliyolenga kumrejeshea ushawishi wake katika eneo hilo badala yake ilionyesha kuwa angali na kibarua kikubwa kufikia lengo hilo huku ikionekana kuchochea migawanyika zaidi miongoni mwa viongozi.
Japo Dkt Ruto alidai bado ndiye “mfalme” wa siasa za eneo hilo wadadisi wanasema ushawishi wa aliyekuwa Naibu wake Rigathi Gachagua ulionekana kumpokonya taji hilo.
“Urafiki wangu na eneo hilo umejengwa kwa zaidi ya miaka 20. Hakuna anayeweza kunitenganisha na watu wa Mlima Kenya,” akasema juzi Naromoru, eneo bunge la Kieni, kaunti Nyeri huku akionekana kumrejelea Bw Gachagua.
“Kwa sababu mlinipigia kura, nitawafanyia kazi hawa hao manabii wa uwongo waaibike,” Dkt Ruto akaongeza.
Rais alipata mapokezo mseto; akilakiwa vizuri katika kaunti za Laikipia na Meru huku akipewa mapokezi vuguvugu katika kaunti za Nyandarua na Kiambu.
Baadhi ya wabunge walioandamana naye, akiwemo kiongozi wa wengi Kimani Ichung’wah, walizomewa katika vituo kadhaa, ishara kwamba hali bado sio shwari kwa Dkt Ruto, kisiasa katika eneo hilo.
Kulingana Profesa Gitile Naituli, ajenda kubwa ya Rais Ruto katika ziara yake haikuwa maendeleo, alivyodai, bali taswira kwamba alilakiwa na watu wengi.
Dkt Ruto ajiulize ni kwa nini mbunge huyo ambaye ni mwandani wake wa karibu alizomewa hata katika kaunti ya Kiambu, anakotoka – Herman Manyora, mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Kenyatta
“Uhalisia wa mambo ni kwamba ziara ya Ruto haikufaulu kuondoa hisia na dhana kwamba aliwasaliti wakazi wa Mlima Kenya na kwamba Bw Gachagua ndiye ‘mfalme’ wa siasa za eneo hilo wakati huu,” anaeleza.
Kulingana na msomi huyo, kwa misingi ya ushauri kutoka kwa Bw Gachagua, wengi walichukulia ziara hiyo kama nafasi ya wao kuvuna pesa kupitia wandani wa Rais Ruto.
“Hii ndio maana juzi, mbunge wa Githunguri Gathoni Wamuchomba alipendekeza kuwa Rais Ruto anafaa kuzuru eneo hilo kila mwezi ili wakazi wafaidike kwa pesa kutoka kwa serikali,” Profesa Naituli anaeleza.
Kwa upande wake, mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Andrew Maringa anasema Bw Gachagua angali anahusudiwa na wakazi kwa sababu anajinadi kama mtetezi wa masilahi ya wakazi wa Mlima Kenya.
“Japo ajenda ya maendeleo ya Rais Ruto ni muhimu, imegubikwa na hisia za wakazi wengi kwamba kwa kumtimua Bw Gachagua na kumkumbatia Raila Odinga, analenga kulitenga eneo hilo kimaendeleo,” anaeleza.
Naye mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Nairobi Herman Manyora anasema kuzomewa kwa Bw Ichung’wah mbele ya Rais Ruto ni ishara kwamba wakazi hawamheshimu hata yeye, kiongozi wa taifa.
“Dkt Ruto ajiulize ni kwa nini mbunge huyo ambaye ni mwandani wake wa karibu alizomewa hata katika kaunti ya Kiambu, anakotoka, tukio ambalo halikushuhudiwa kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022. Rais ajue kwamba hali sio nzuri kwake katika eneo la Mlima Kenya na kwamba ziara yake haikuwa na umuhimu wowote kwake kisiasa,” anaeleza akisema kuwa Gachagua angali mwenye ushawishi Mlima Kenya.
Bw Manyora anatoa mfano wa fujo zilizolipuka juzi wakati wafuasi wa Bw Gachagua na wale wa Mbunge wa Mathira Eric Wamumbi walipopigana katika ibada ya mazishi ya Anne Wanjiru Mumbuchi katika Shule ya Msingi ya Muragara, kaunti ya Kirinyaga.
Wafuasi wa Bw Gachagua walikasirishwa na matamshi ya Bw Wamumbi yaliyomdhalilisha naibu huyo wa rais wa zamani.
Bw Wamumbi ni mmoja wa wandani wa Rais Ruto katika eneo hilo na ni mmoja wa waliofanya maandalizi na mapokezi ya kiongozi wa taifa Mlima Kenya.