Habari

Mbunge aliyerekodi wenzake wakipigana kuadhibiwa kwa kuaibisha taasisi

Na SAMWEL OWINO April 14th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

MBUNGE ambaye alirekodi video ya wenzake wawili wakipigana Jumanne wiki iliyopita, huenda atakabiliwa na adhabu kali kwa kuanika Bunge la Kitaifa na kuaibisha asasi hiyo.

Taifa Leo imebaini kuwa uchunguzi ambao unashirikisha polisi wa bunge na walinzi bungeni tayari wamemtambua mbunge huyo.

Ripoti ya uchunguzi inatarajiwa kuwasilishwa kwa Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetangúla wiki hii ambapo atatoa mwelekeo kuhusu suala hilo.

Duru kutoka Bungeni zimearifu kuwa uongozi wa bunge umekasirishwa na kurekodiwa kwa video hiyo na mbunge huyo huenda akapokezwa adhabu kali kwa mujibu wa kanuni za bunge.

Inadaiwa mbunge huyo alitoa video hiyo kwa jamaa yake ambaye ni mwanablogu ilhali sheria za bunge zinaharamisha kurekodiwa kwa video bungeni.

“Mbunge aliyerokodi video yupo matatani zaidi hata kuliko wale waliopigana kwa sababu hatua yake ilisawiri bunge vibaya na kuaibisha asasi hiyo. Ingawa waliopigana wameomba msamaha, aliyerekodi video hiyo bado hajafanya hivyo,” ikasema duru hizo.

Mbunge wa Mavoko Patrick Makau ambaye ni mwanachama wa Tume za Huduma za Bunge (PSC) alisema kuwa alimwona aliyerekodi video hiyo na atasaidia polisi kwenye uchunguzi.

Akiomba Bunge msamaha, mbunge mteule Umulkher Harun ambaye alipigana, alidai kuwa Mbunge wa Tigania Mashariki Mpuri Aburi ndiye alirekodi tukio hilo.

“Nilimwona Mheshimiwa Aburi akirekodi na nikamwendea kumwambia asifanye hivyo,” akasema Bi Harun.

Mbunge anayehudumu kwenye Bunge la Afrika Mashariki Iman Falhada ambaye alipigana na Bi Harun alipigwa marufuku kufika kwenye majengo ya bunge kwa siku 90.