Makala

Mwenendo hatari waibuka polisi wakiwauzia raia vitoa machozi

Na RUSHDIE OUDIA April 15th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MIHEMKO mikali ya kisiasa inayoandamana na ghasia imeanza kuchipuza nchini, huku kukishuhudiwa mwenendo hatari ambapo vitoa machozi vinapatikana mikononi mwa raia.

Maswali yameibuka jinsi raia hupata silaha hizo hatari au nani huwasaidia kuzipata kwa urahisi.

Sababu ni kwamba vitoa machozi hutumika mahsusi na walinda usalama kuwatawanya watu wanaozua fujo kwenye mikutano ya hadhara, haswa ile ya kisiasa.

Mnamo Aprili 9, mwanamume mmoja alikamatwa katika eneo la Nyakach, Kaunti ya Kisumu akiwa njiani kuvuruga chaguzi za chama cha ODM, ngazi ya kaunti ndogo katika kambi ya Chifu ya Kodingo.

Polisi walimpata na mikebe ya vitoza machozi na silaha kama vile visu na panga.

Wenzake wanne walifaulu kutoroka.

Siku hiyo hiyo, umbali wa kilomita 108 kutoka mjini wa Bondo, Kaunti ya Siaya, polisi walisimamisha gari moja lililokuwa likiendeshwa vibaya karibu na makutano ya barabara ya Koyucho.

Walipolifanyia msako, walipata bastola bandia na vitoa machozi.

Afisa wa polisi aokota mkebe wa kitoa machozi katika maandamano yaliyopita. Picha|Billy Ogada

Polisi wanaamini kuwa silaha hizo zililenga kutumiwa kuvuruga chaguzi za ODM katika eneo hilo.

Kamanda wa polisi katika Kaunti Ndogo ya Bondo Bw Robert Aboki, alithibitisha kukamatwa kwa watu wawili waliokuwa wakisafiri kwa gari hilo aina ya Toyota Passo.

“Tunaendesha uchunguzi ili kubaini walikopata vitoa machozi na nia yao,” akasema na kuongeza:

“Aidha tunasubiri mmiliki wa gari hilo ajitokeze ili tumjue.”

Lakini duru zinasema kuwa visa kama hivi vinaendelezwa na maafisa wa polisi watundu na watu wenye ushawishi kisiasa.

Taifa Leo iliongea na maafisa mbalimbali katika huduma ya kitaifa ya polisi, ambao walifichua kuhusu biashara ya vitoa machozi inayoendelea katika huduma hiyo.

Sakata hiyo inashirikisha maafisa wa polisi wafisadi, wanasiasa walaghai na raia wasioheshimu sheria.

Afisa mmoja wa polisi, ambaye aliomba tulibane jina lake, aliungama kwamba baadhi ya wenzake wamekuwa wakiwauzia raia vitoa machozi.

“Ukipewa mikebe 10 kudhibiti umati wa watu, unatumia tatu na badala ya kurejesha saba, unarejesha mbili na kusalia na tano. Hamna atakayekuuliza swali lolote,” akaeleza.

“Tofauti na bunduki, mikebe ya vitozi machozi haina nambari maalum, na hivyo sio rahisi kuitambua,” afisa huyo akaongeza.

Kulingana na afisa huyo, baadhi ya waandamanaji pia hukusanya mikebe ya vitoa machozi ambayo haijalipuka na kuiweka kwa matumizi nyakati zingine.

“Kuna maafisa wengine wa polisi ambao hupenda kujionyesha. Wao hubeba vitoa machozi ndani ya magari yao wakilenga kuwafurahisha marafiki zao au watu wa familia zao, bila kung’amua hatari wanayojiwekezea,” akaongeza.

Afisa mwingine wa kampuni ya kibinafsi ya ulinzi, ambaye hutoa huduma zake kwa wanasiasa na wageni wengine mashahuri, alisema maafisa wakuu wa polisi hufahamu kuhusu sakata hiyo.