Habari

Wabunge washtuka kuambiwa Ruku, anayetaka uwaziri, hakulipa kodi ya nyumba 2021

Na COLLINS OMULO April 15th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WAZIRI Mteule wa Utumishi wa Umma Geoffrey Ruku, jana alikabiliwa na wakati mgumu kujitetea kuhusu madai ya kufeli kulipa kodi ya nyumba ya Sh460,000, kudhamini mswada tatanishi na miegemeo yake ya kisiasa alipofika mbele ya wabunge kuhojiwa kwa wadhifa huo.

Mbunge huyo wa Mbeere Kaskazini pia alikuwa na wakati mgumu kujibu maswali mbele ya Kamati ya Bunge kuhusu Uteuzi ikizingatiwa kuwa hajawahi kuhudumu katika sekta ya umma na ufahamu finyu wa majukumu ya wizara hiyo.

Bw Ruku pia alishutumiwa kwa kuonyesha wazi mapendeleo alipohudumu kama mbunge pale alipounga mkono ushuru wa magari uliopendekezwa katika Mswada wa Fedha wa 2024 uliozimwa mwaka jana.

Wanachama wa kamati hiyo inayoongozwa na Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula, walimwekea presha, wakitaka kujua jinsi miegemeo kama hiyo itaathiri utekelezaji wa majukumu yake endapo uteuzi wake utaidhinishwa.

Shughuli ya kumpiga msasa Bw Ruku ilianza kwa kuangaziwa kwa mvutano kati yake na mmiliki wa nyumba aliyoishi zamani.

Waziri huyo mteule alilaumiwa kwa utovu wa maadili, utovu wa uwajibikaji wa kifedha, mienendo potovu na kudharau mahakama na kutokuwa mwaminifu, kamati hiyo ilipoambiwa kuwa alifeli kulipa kodi ya nyumba, ada za maji na umeme.

Aidha, mwenye nyumba alidai kuwa Bw Ruku alisababisha uharibifu mkubwa kwa nyumba hiyo ya makazi aliyokodisha jijini Nairobi.

“Bw Ruku alifeli kulipa kodi ya nyumba ya kima cha Sh460,000. Aliomba muda zaidi wa kulipa akidai mamake alikufa mnamo Juni 2021 ilhali mamake alikufa baadaye mnamo Oktoba 2021,” ikasema taarifa iliyowasilisha kwa kamati hiyo na mlalamishi huyo.

“Mlalamishi amepata hasara ya zaidi ya Sh1 milioni kutokana na mienendo ya Ruku. Kwa hivyo, tunatoa wito kwa kamati kuzingatia kesi inayoendelea kuhusu suala hilo na ikatae kumwidhinisha kwa wadhifa aliopendekezwa kuhudumu,” hati hiyo ya malalamishi ikaeleza.

Kwa upande wake, Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Kimani Ichung’wah, alimtaka Bw Ruku kufafanua ikiwa kweli amewahi kumlaghai mtu yeyote kuhusiana na kodi ya nyumba au suala jingine.

“Sijafeli kulipa kodi au kulaghai mtu yeyote kuhusu kodi au suala lolote linalohusiana na biashara ya kibinafsi. Kuna watu ambao wangetaka kulaghai kwa misingi ya hadhi yako na sasa wanaibua madai mengi ambayo hayana msingi wowote,” akasema Bw Ruku.

Hata hivyo, aliiomba Kamati hiyo imruhusu kutolizungumzia zaidi suala hilo kwa sababu bado linashughulikiwa mahakamani.

Bw Ichung’wah ambaye ni Mbunge wa Kikuyu pia alimsukuma Bw Ruku kuhusu hali kwamba hajawahi kufanya kazi katika utumishi wa umma, akimuuliza ikiwa ataweza kutekeleza majukumu ya wizara hiyo “ikizingatiwa kuwa umehudumu kwa miaka mwili pekee kama Mbunge.”

“Watu wasio na tajriba ya miaka mingi katika utumishi wa umma huwa wajeuri huku wakiwachukia na kuwadharau wabunge. Je, tutashuhudia tabia kama hiyo na dharau, ambazo tumeona nyakati zilizopita, kutoka kwako endapo tutakuidhinisha kwa wadhifa huu?” Bw Ichung’wah akauliza.