Miili ya vijana wawili waliokufa maji ufukweni Shella, waopolewa
MIILI ya vijana wawili kati ya watatu walioripotiwa kutoweka baharini eneo la Shella, Kaunti ya Lamu, ilipatikana Jumatatu ikielea karibu na ufuo huo huo wa Shella.
Akithibitisha taarifa hizo, Meneja wa Kituo cha Kukabiliana na Majanga ya Dharura Lamu (EOC), Iftakhar Majid, alisema miili hiyo ilipatikana kufuatia operesheni inayoendelea ya kuwasaka waliotoweka wakati wakiogelea baharini ufuoni Shella mnamo Jumapili jioni.
Bw Majid alisema kwa sasa operesheni bado inaendelea ili kuusaka mwili wa tatu. Vijana hao walikuwa miongoni mwa kundi la wana-rika 30 waliokuwa wamezuru Lamu kutoka eneo la Hongwe, tarafa ya Mpeketoni kwa shughuli za kikanisa.
Baada ya kukamilisha shughuli zao za kanisa mapema Jumapili, waliandamana hadi ufuo wa Shella ili kujivinjari kwa kuogelea. Hali ilibadilika ghafla pale watatu waliokuwa miongoni mwa makumi ya walioogelea waliposhindwa nguvu, hivyo kutoweka baharini.
“EOC ilipokea simu kutoka kwa msamaria mwema aliyetufahamisha kilichokuwa kikiendelea Shella. Ilikuwa majira ya saa 12 unusu hivi jioni ya Jumapili. Tulifika eneo husika na kuanzisha msako mara moja lakini tulikatiza operesheni katikati baada ya giza kusheheni kwani usiku ulikuwa umewadia,” akasema Bw Majid.
Operesheni ya kusaka miili ya watatu hao hata hivyo ilirejelewa Jumatatu asubuhi, hivyo kupelekea kuopolewa kwa miwili ambayo ni ya mwanaume na mwanamke.
Operesheni inaendelezwa na maafisa wa kituo cha EOC Lamu kwa ushirikiano na Kenya Coast Guard Service (KCGS), Shirika la Msalaba Mwekundu nchini na wapiga mbizi wa kujitolea.
“Kwa sasa operesheni bado inaendelea kuusaka mwili wa tatu na wa mwisho. Ningeshauri watalii, wageni na wenyeji kuwa makini wanapoogelea kwenye fuo zetu. Baadhi ya fukwe, ikiwemo Shella, ni hatari kwa usalama wao kwani zimesheheni vidimbwi vya kina kirefu,” akasema Bw Majid.
Pia aliwataka wavuvi na mabaharia wengine kuwa makini na kutii maonyo ya kila mara yanayotolewa na ofisi yake na ile ya Idara ya Hali ya hewa kuhusiana na hali ilivyo baharini.
Si mara ya kwanza watu kufa maji wakati wakiogelea kwenye ufukwe wa Shella, Lamu.
Julai 2018, mwanafunzi wa Taasisi ya Mafunzo na Kiufundi (TVET) ya Lamu, Juma Mohamed, alikufa maji wakati akiogelea Shella.
Novemba 2018, kijana wa miaka 25 kwa jina Joseph Kitsao, pia alikufa maji akiogelea kwenye ufukwe wa Shella.
Wenzake wawili waliokolewa na wapiga mbizi wa kujitolea waliokuwa karibu wakati wa tukio.
Mbali na Shella, sehemu zingine zinazotambuliwa kuwa hatari kwa kuogelea na hata kuvuka ukisafiri kwenye Bahari Hindi, Kaunti ya Lamu ni vivuko vya Mkanda, Manda Bruno, Mlango wa Kipungani, vyote vikipatikana Lamu Magharibi.
Vingine ni Mlango wa Tanu huko Mkokoni, Mlango wa Ali upatikanao Kiwayu na Mlango wa Bomani ulioko Kiunga, vyote vikiwa Lamu Mashariki.