Ni gozi la kukanyaga mtu shingo UEFA
MADRID, UHISPANIA
REAL MADRID wana kazi ngumu kubadilisha matokeo ya mkondo wa kwanza watakapoalika Arsenal leo usiku katika pambano la marudiano la robo fainali ya michuano ya Klabu Bingwa barani Ulaya.
Vigogo hao ambao ndio mabingwa watetezi wa kombe hilo walicharazwa 3-0 timu hizo zilipokutana ugani Emirates katika mkondo wa kwanza ambapo kiungo mahiri Declan Rice alishangaza wengi kwa kupachika wavuni mabao mawili kutokana na mikwaju ya ikabu, huku jingine likifungwa na Mikel Merino.
Kwingine, Bayern Munich watakuwa na kibarua cha kufuta kichapo cha 2-1 watakapokuwa ugenini kurudiana na Inter Milan kwenye robo fainali nyingine.
Kikosi hicho cha kocha Vincent Kompany kilitawala mkondo wa kwanza lakini kikashindwa kutumia vyema nafasi nyingi za wazi.
Mwishoni mwa wiki, vigogo hao waliagana kwa sare ya 2-2 na mahasidi wao Borussia Dortmund katika pambano la Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) huku Inter ikicharaza Cagliari kwenye mechi ya Ligi Kuu ya Italia (Serie A).
Akizungmza kuhusu mechi kati ya Madrid na Arsenal, aliyekuwa nahodha wa Manchester United, Rio Ferdinand amesema kikosi hicho cha Mikel Arteta kina nafasi kubwa ya kushinda mechi hiyo na kufuzu kwa nusu fainali.
Jagina hiyo amebashiri kuwa Arsenal itafunga bao moja ambalo litawachanganya wenyeji ambao wanahitaji ushindi wa 4-0 ili kusonga mbele.
Hata hivyo, mlinzi huyo mstaafu wa kimataifa ameonya kwamba huenda Arsenal wakakumbwa na wakati mgumu ikiwa watakubali kufungwa mapema.
“Kwa jumla, nadhani Arsenal watasonga mbele. Wana nafasi kubwa dhidi ya asilimia 4 ya Real Madrid ambao walichanganyikiwa katika mkondo wa kwanza. Kikosi cha Madrid kimekuwa na matatizo ya kutoelewana kwa muda mrefu.”
“Kurejea kwa Bukayo Saka kumeongezea Arsenal nguvu, kwani amebadilisha kila kitu kikosini. Kama asingekuweko, sidhani wangeshinda kwa mabao 3-0. Kwa sababu hiyo, ninaamini Arsenal watafuzu.”
“Licha ya kuwa na matumaini hayo makubwa, ningependa kuwashauri Arsenal wajihadhari na umati mkubwa utakaojaza uga wa Santiago Bernabeu kuwachanganya akili. Iwapo Arsenal watatoboa, huenda wakashinda kombe hilo kwa mara ya kwanza.”
Arsenal wanaingia uwanjani baada ya mwishoni mwa wiki kutoka sare ya 1-1 na Brentford katika mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) iliyochezewa Emirates.
Madrid kwa upande wake ilibidi wapigane vikali kabla ya kuondoka na ushindi wa 1-0 dhidi ya Alaves katika pambano la La Liga, Jumapili, kwenye mechi ambayo Kylian Mbappe alipigwa kadi nyekundu baada ya kucheza ngware.
The Gunners hawajashindwa katika mechi tatu dhidi ya Real Madrid katika michuano ya Klabu Bingwa (UCL), mbali na kutofungwa bao na wapinzani hao.
Kichapo cha 3-0 kutoka kwa Arsenal ni cha kwanza katika hatua ya muondoano kwa mabao matatu. Waliwahi tu kubadilisha matokeo katika hatua hii mara moja dhidi ya Derby County msimu wa 1975-76.
Los Blanco wamecheza na klabu za Uingereza mara 53 katika michuano hii ya bara Ulaya, na kushindwa kwa zaidi ya mabao matatu mara mbili pekee, 5-1 dhidi ya Derby (1975-76) na 4-0 dhidi ya Tottenham Hotspur msimu wa 2010-11.
Aurelien Tchoumeni aliyekosa mkondo wa kwanza kutokana na adhabu ya kadi anatarajiwa kurejea, pamoja na Dani Ceballos na Ferland Mendy.
Eder Militao amerejea mazoezini lakini hajapata nafuu kikamilifu. Camavinga aliyepigwa kadi nyekundu dakika za mwisho ugani Emitares ataikosa mechi ya leo.
Huenda Arsenal watacheza bila Ben White, Takehiro Tomiyasu, Kai Havertz, Gabriel Magalhaes na Gabriel Jesus, lakini Riccardo Calafiori amerejea kikosini baada ya kupata nafuu.
Ratiba ya Jumatano usiku
Real Madrid vs Arsenal (10pm),
Inter Milan vs Bayern Munich (10pm)