Mvua ya gharika itakaribisha msimu wa Pasaka, wataalamu waonya Wakenya
IDARA ya Utabiri wa Hali ya Hewa nchini imetoa tahadhari kwa Wakenya kuhusu mvua kubwa itakayonyesha katika maeneo mbalimbali ya nchi kwa kipindi cha siku saba kuanzia Jumanne, Aprili 15 hadi Jumatatu, Aprili 21.
Mkurugenzi wa Idara ya Hali ya Hewa, Dkt David Gikungu, alisema kuwa mvua hiyo itakayoambatana na ngurumo za radi inatarajiwa hasa wakati wa alasiri na usiku, huku baadhi ya maeneo yakitarajiwa kupata mvua nyepesi asubuhi kabla ya hali ya jua kuchomoza kwa muda mfupi.
“Mvua ya asubuhi itashuhudiwa katika maeneo machache, ikifuatiwa na vipindi vya jua. Hata hivyo, mvua kubwa na ngurumo za radi inatarajiwa alasiri na usiku katika sehemu nyingi,” alisema Dkt Gikungu.
Miongoni mwa maeneo yatakayoathirika zaidi ni milima ya magharibi na mashariki mwa Bonde la Ufa, Bonde la Ziwa Victoria, maeneo ya chini kusini-mashariki, na kaskazini-mashariki mwa nchi.
Katika eneo la Kati mwa Kenya, hususan kaunti za Nyandarua, Laikipia, Nyeri, Kirinyaga, Murang’a, Kiambu, Meru, Embu, Tharaka Nithi, na jiji la Nairobi, wakazi wametahadharishwa kujiandaa kwa mvua usiku na baridi kali.
Idara ilisema kuwa viwango vya joto usiku katika maeneo haya vitashuka hadi chini ya nyuzi joto 9, hali inayoweza kuathiri watoto, wazee, na wagonjwa.
Kaunti za Siaya, Kisumu, Homa Bay, Migori, Kisii, Nyamira, Trans Nzoia, Baringo, Uasin Gishu, Elgeyo-Marakwet, Nandi, Nakuru, Narok, Kericho, Bomet, Kakamega, Vihiga, Bungoma, Busia, na Pokot Magharibi pia zimo kwenye orodha ya maeneo yanayotarajiwa kupokea mvua kubwa.
Hali kama hiyo inatarajiwa katika kaunti za Kitui, Makueni, Machakos, Kajiado, Taita Taveta, na sehemu za ndani za Tana River, ambako asubuhi kutakuwa na mawingu na mvua nyepesi kabla ya hali ya mvua kubwa kuanza alasiri na kuendelea hadi usiku.
Wakati mvua zikitawala maeneo mengi, kaunti za Mombasa, Kilifi, Lamu, Kwale, Marsabit, Mandera, Wajir, Garissa, na Isiolo zimetabiriwa kupata joto kali la mchana hadi kufikia nyuzi joto 33.
Wataalamu wa hali ya hewa wamewahimiza wananchi kuwa waangalifu na kufuata ushauri wa serikali, hasa wale wanaoishi maeneo yenye historia ya mafuriko, maporomoko ya ardhi, na miundombinu dhaifu.