Wahudumu wa biashara ya mapenzi wahofia maisha kufuatia uhaba wa kondomu
UHABA mkubwa wa kondomu na dawa za kuzuia maambukizi ya virusi vya Ukimwi kabla ya mtu kuambukizwa (PrEP) katika jiji la Nakuru na miji mingine unahatarisha vita dhidi ya Ukimwi na magonjwa mengine ya zinaa nchini Kenya.
Huduma za bure katika hospitali na vituo vya afya kusaidia makundi maalum kama wafanyabiashara wa ngono zimekwama baada ya bidhaa hizo muhimu kukosekana.
Uhaba huo umeweka hatarini afya na maisha ya zaidi ya wafanyabiashara wa ngono 4,000 wanaofanya kazi katika barabara kuu ya Nairobi-Nakuru-Eldoret — hususan maeneo ya Mai Mahiu, Longonot, Naivasha, Gilgil, Kikopey, Pipeline, Salgaa na Sachangwan.
Barabara hii ni kiungo muhimu katika usafiri katika Barabara Kuu inayounganisha Kenya na mataifa kama Uganda, Sudan Kusini, Rwanda na Burundi. Kwa sababu hiyo, mtangusano wa madereva wa malori na wafanyabiashara wa ngono huongeza hatari ya maambukizi ya Ukimwi.
Mwenyekiti wa kundi la Smart Ladies, linalowakilisha wafanyabiashara wa ngono katika eneo hilo, Bi Daisy Achieng, alieleza hali kuwa ya dharura.
“Kuna uhaba mkubwa wa kondomu na dawa za PrEP. Vituo vyote ambavyo tulikuwa tukitegemea havina tena. Serikali lazima iingilie kati kwa haraka,” alisema.
Wanafunzi, vijana, na wanaharakati wengine pia wamelalamikia hali hiyo na kuitaka serikali kushughulikia tatizo hilo haraka ili kulinda afya ya umma.
“Kama wanafunzi, tunahofia maisha yetu. Ikiwa tungekuwa na uhakika wa usalama wa kiafya, tunaweza kuzingatia masomo vyema,” alisema Paul Kamau wa Chuo Kikuu cha St Paul, Nakuru.
Afisa wa Afya wa Kaunti ya Nakuru, Bi Roselyn Mungai, alisema kuwa serikali ya kaunti inatathmini upya mipango yake ya afya kufuatia kujiondoa kwa shirika la USAID katika kufadhili miradi ya kuzuia Ukimwi na magonjwa mengine.
“Tunalenga kuimarisha mpango wa kuzuia Ukimwi, kifua kikuu na afya ya familia bila kutegemea misaada ya kigeni,” alisema.
Kwa siku mbili zilizopita, wataalamu kutoka Shirika la Kitaifa la Kudhibiti Ukimwi na Magonjwa ya Zinaa (NASCOP) waliwasiliana na maafisa wa afya ya umma wa kaunti hiyo wakilenga makundi yaliyo hatarini kama wanaume wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja, watu wanaojidunga dawa, na watu waliobadili jinsia.
Dkt Reuben Osiemo, afisa wa afya ya umma, alisisitiza kuwa matumizi ya kondomu kwa asilimia mia moja yamechangia kupunguza maambukizi ya Ukimwi na mimba zisizopangwa.
“Tunahitaji suluhisho la haraka ili kurejesha usambazaji wa bidhaa hii muhimu. Kondomu ni zana rahisi na iliyothibitishwa ya kuzuia maambukizi,” alisema Dkt Osiemo.
Kenya huhitaji takriban kondomu milioni 400 kila mwaka. Serikali husambaza takriban nusu tu ya kiwango hicho. Mipango ya kutoa kondomu bure ilizinduliwa mwaka wa 2001 ikitegemea misaada kutoka kwa wahisani
Kwa sasa, wadau wanatoa wito kwa serikali kuanzisha mfumo ambapo watu wa kipato cha kati na juu wananunua kondomu kwa bei nafuu, huku wale wa kipato cha chini wakisaidiwa kupitia usambazaji wa bure.
Kundi la Smart Ladies linasisitiza kuwa mafanikio yaliyopatikana kwa miongo miwili iliyopita hayawezi kudumishwa bila uwekezaji wa serikali katika huduma za kinga.
“Tuliungana mwaka 2015 baada ya mauaji ya kiholela dhidi ya wafanyabiashara wa ngono. Leo tunapaza sauti tena kwa ajili ya maisha yetu,” alisema Bi Achieng.