Soko la mitumba lahamia TikTok wafanyabiashara wakisema imewabadilishia maisha
KWA muda mrefu, biashara ya mitumba ilihusishwa na vibanda vya Gikomba jijini Nairobi au Kongowea mjini Mombasa, ambapo wanunuzi walizoea kuchagua bidhaa kwa jasho na vumbi.
Lakini hali hiyo sasa imebadilika—mitumba imeingia mtandaoni, na TikTok imegeuka kuwa soko kuu la kisasa.
Katika mitandao hiyo, bidhaa kama mikoba ya wabunifu maarufu, mazulia, shuka na mavazi ya ofisi huuzwa moja kwa moja kupitia jukwa hilo, huku wauzaji wakifuatwa na maelfu ya wateja wanaotazama kwa wakati mmoja.
Mauzo hufanyika papo kwa hapo; anayesema “kwangu” wa kwanza, ndiye anayepata.
Alex Kimani, anayejulikana kibiashara kama Jamal, ni mmoja wa vijana waliogeuza TikTok kuwa jukwaa la mafanikio. Kila siku asubuhi, hupatikana sokoni Gikomba, akichagua mikoba ya mitumba kwa umahiri wa hali ya juu.
“Tiktok ndiyo imenijenga kama chapa. Bila hiyo, duka langu lisingekuwepo,” asema Jamal, ambaye kila upeperushaji huanza na sala ya pamoja na wafuasi wake mtandaoni.
Jamal alianza biashara hii baada ya kuacha masomo ya usanifu. Alianza kama kuuza mikoba kwa wamiliki wa maduka ya mtandaoni jukumu linalofahamika kama runner katika uuzaji wa dijitali. “Nilikuwa natuma ujumbe kwa kurasa zaidi ya 100, lakini waliokuwa wakinijibu walikuwa wawili tu,” asema.
Mwaka wa 2023, aliamua kujaribu bahati kwenye TikTok.
“Video yangu ya kwanza ilipendwa mara 2,000. Niliposikia kina dada wakisema nianze kuenda live, niliamua kujaribu. Baada ya mara ya kwanza, nilipata pesa ambazo sikuwa nimepata mbeleni.”
Sasa, Jamal hununua mikoba ya kiwango cha juu, akihakikisha kila bidhaa ni halali na ya kuvutia.
“Ninashughulikia usafi, kufumua, na kuthibitisha ubora wa kila bidhaa. Siko tayari kuuza bidhaa iliyochakaa.”
Esther Kwamboka, anayejulikana mtandaoni kama Elsie, aliacha kazi ya benki na kuwekeza katika biashara ya mazulia, shuka na taulo za mitumba mjini Kisii.
“Niliamua kuchukua hatari. Nilihisi biashara inanivutia,” asema.
Elsie huuza ndani ya Kisii, lakini pia hupakia mzigo kwenda miji mingine na hata mataifa ya ng’ambo. “Nina wateja Amerika, Uingereza, Nairobi, Nyeri, hata Nanyuki,” asema.
Biashara yake huendeshwa kwa kutumia video za TikTok na picha anazosambaza kupitia WhatsApp. “Napakia video zaidi ya kumi kwa siku. TikTok ndiyo uwekezaji wangu mkuu.”
Deborah Munywoki alipoteza kazi wakati wa janga la corona mwaka 2020. Alitumia fursa hiyo kuingia kwenye biashara ya mitumba ya mavazi ya wanawake.
“Kwanza nilianza na mikoba, lakini baadaye nikahamia mavazi rasmi. Niliona hiyo ndiyo nafasi yangu ya kujitofautisha,” asema.
Baada ya kuzichagua bidhaa sokoni, huwa anazirekebisha, kuzipanga na kuziuza moja kwa moja kupitia TikTok kuanzia jioni hadi usiku wa manane.
“Nauza zaidi nikiwa live TikTok. Wateja huangalia, wanapenda, na kununua moja kwa moja,” asema Deborah.
“TikTok imenibadilishia maisha,” asema.