‘SOFT LIFE’: Gen Z hawajui kubana pesa na kujinyima, ripoti yaonyesha
KIZAZI cha Gen Z, cha watu waliozaliwa kati ya mwaka 1997 hadi 2012, kimeibuka kuwa kundi lenye ushawishi mkubwa zaidi kiuchumi nchini Kenya, kikitarajiwa kutumia zaidi ya Sh4.4 trilioni mwaka wa 2025 pekee.
Takwimu hizi zimetolewa na shirika la World Data Lab (WDL) kupitia ripoti yake mpya; “Gen Z na hali ya baadaye ya matumizi ya fedha Afrika.”
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, zaidi ya Wakenya milioni 17 wa kizazi cha Gen Z hutumia fedha nyingi zaidi kwenye chakula, makazi na usafiri.
Miji ya Nairobi, Mombasa na Kisumu imetajwa kuongoza kwa matumizi hayo mwaka huu, huku Meru, Thika na Ruiru ikitajwa kama miji inayokua kwa kasi zaidi katika matumizi ya kizazi hiki kufikia mwaka 2035.
WDL inaeleza kuwa Nairobi inaongoza kwa matumizi ya fedha ya Gen Z barani Afrika kwa kiwango cha dola 10.1 bilioni (1.3 trilioni), ikifuatiwa na Mombasa kwa kasi ya ukuaji wa asilimia 8.2. Miji ya Meru (asilimia 10.1), Thika (asilimia 8.1) na Ruiru (asilimia 7.9) imetambuliwa kama vituo muhimu vinavyoibuka kiuchumi kwa kizazi hiki.
Kenya imetajwa kuwa nchi ya tano kwa ukubwa wa uchumi wa Gen Z barani Afrika, ikifuatia Nigeria, Misri, Afrika Kusini na Ethiopia.
Hali hii inaonyesha kwamba nguvu ya uchumi wa Kenya kwa sasa imejikita zaidi mijini, ambako kuna miundombinu bora, ajira na upatikanaji wa huduma za kidijitali.
Ripoti hiyo pia inatabiri kuwa kufikia mwaka 2040, Gen Z watasalia kuwa kundi kuu la watumiaji huduma na bidhaa, hata kama kizazi cha Alpha (kilichozaliwa baada ya 2012) kitaongoza kwa idadi ya watu.
Kwa sasa, Gen Z ndio kundi lenye uwezo mkubwa wa kifedha, likiwa na uwezo mkubwa wa kutumia fedha kununua bidhaa ikilinganishwa na wazazi wao.
Mkurugenzi Mtendaji wa World Data Lab, Wolfgang Fengler, alisema: “Gen Z kwa sasa ndio kundi kubwa zaidi la kiuchumi barani Afrika.”
Wana matumizi ya juu zaidi na wanatarajiwa kufikia dola 801 bilioni (Sh103 trilioni) mwaka huu, na zaidi ya trilioni moja baada ya mwaka 2032.”
WDL inaonya kuwa iwapo biashara na serikali hazitabadilika ili kufanikisha mahitaji na matarajio ya kizazi hiki, kuna hatari ya kutokea kwa mgawanyiko mkubwa wa kiuchumi na kijamii.
Kampuni na taasisi za serikali zimetakiwa kurekebisha mikakati yao, ikiwemo njia za mawasiliano, upatikanaji wa bidhaa, na uzoefu wa wateja ili kufikia matakwa ya kizazi cha kidijitali, chenye uelewa mkubwa wa teknolojia, na ambacho kinahitaji huduma za haraka zilizobinafsishwa.
“Uchunguzi wetu unaonyesha hitaji la dharura kwa kampuni na taasisi kubadilisha mbinu zao, ili kushirikiana na kizazi hiki kinachounda msingi mpya wa matumizi ya bidhaa na huduma Afrika nzima.”
Ripoti hiyo imejiri wakati ambapo uchumi wa Kenya unakabiliwa na changamoto ya gharama ya maisha, lakini Gen Z wanaonekana kuendelea kuwa kundi lenye matumizi makubwa.