Habari

Wakazi wateketeza gari la padre kwa tuhuma za wizi na uasherati

Na GEORGE ODIWUOR April 16th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

MAAFISA kutoka Idara ya Uchunguzi wa Jinai (DCI) eneo la Rachuonyo Mashariki, Kaunti ya Homa Bay, wameanzisha uchunguzi baada ya watu wenye hasira kuteketeza gari la mhubiri wa eneo hilo kwa tuhuma za wizi.

Wakazi hao waliokasirika baada ya kuliona gari hilo barabarani nyakati za usiku walimtuhumu padre huyo kutumia gari lake kwa wizi wa mifugo na kujihusisha na mapenzi nje ya ndoa.

Kamanda wa Polisi wa Rachuonyo Mashariki Laban Omol alithibitisha kwamba DCI inawahoji wakazi ili kubaini kilichosababisha umati huo kuteketeza gari hilo.

“Tumekabidhi kesi hiyo kwa maafisa wa DCI ambao watawahusisha wakazi na kukusanya vidokezo ili kubaini kiini cha kitendo hiki,” alisema Bw Omol, akiongeza kuwa mhubiri huyo alipata majeraha baada ya kushambuliwa na kundi la watu.

Shambulio hilo ni la hivi punde zaidi huku wakazi wakizidi kulenga magari na watu wasiowafahamu kutokana na hofu ya wizi wa mifugo.

Katika miezi michache iliyopita, mkoa huo umeripoti kukithiri kwa visa vya wizi wa mifugo, mara nyingi vikiwahusisha washukiwa kutumia magari kusafirisha mifugo iliyoibiwa.

Mwezi uliopita katika Kijiji cha Nyawango, Kokwanyo Magharibi, mwanamume mmoja aliuawa na mwili wake kuteketezwa baada ya wakazi kumshuku yeye na wenzake kupanga kuiba mifugo.

Kikundi hicho kilipatikana karibu na shamba ambalo mbuzi walikuwa na inadaiwa walikuwa na nambari mbili za usajili.

Siku nne kabla, wanaume wawili waliuawa katika Kijiji cha Katolo, Kitongoji kidogo cha Miriu.

Gari lao lilikuwa limeharibika na hivyo kuzua shaka kwamba walikuwa wakiendesha wizi. Wakazi waliwahoji na baadaye kuwashambulia na kusababisha vifo vyao na hata kuteketeza gari lao.

Washukiwa wengine wawili waliuawa katika Kijiji cha Kakoth, Kitongoji cha Kokwanyo Magharibi mnamo Februari 12 huku wengine wawili akiwemo mwanamke mmoja wakijeruhiwa vibaya baada ya kukamatwa wakirandaranda karibu na boma ambalo mmiliki wake hayupo.