‘Kupitisha bila breaks’: Wabunge waidhinisha Ruku, Cheptumo; wamkingia dhidi ya shutuma
WABUNGE wamemtetea Waziri Mteule wa Jinsia, Utamaduni, Sanaa na Turathi Bi Hannah Wendot Cheptumo kufuatia kauli aliyotoa juzi kwamba baadhi ya wasichana wanaouawa na wapenzi wao wa kiume ni wale ‘wanaosaka pesa’.
Wakiongozwa na kiongozi wa wengi Kimani Ichung’wah na kiranja wa wachache Millie Odhiambo, walimtaja Bi Cheptumo kama mtetezi wa haki za wasichana na wanawake na kwamba hafai kulaumiwa kwa “kuteleza ulimi wake.”
“Ningependa kulihakikishia bunge hili kwamba Bi Cheptumo aliomba msamaha rasmi kwa usemi huo alipokuwa akifanyiwa usaili na Kamati ya Bunge kuhusu Uteuzi Jumatatu, Aprili 14. Vile vile, ameomba msamaha kupitia akaunti yake ya X,” akaeleza mbunge huyo wa Kikuyu.
Bw Ichung’wah alisema hayo bungeni Jumatano, Aprili 16, 2025 alipowasilisha rasmi ripoti ya kamati hiyo iliyoidhinisha Bi Cheptumo kwa uteuzi rasmi kuwa Waziri wa Jinsia.
Bi Cheptumo alijipata motoni Jumatatu alipokuwa akijibu swali la Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula (mwenyekiti wa kamati hiyo ya uteuzi) kuhusu kiini cha visa vya mauaji ya wasichana.
“Inasikitisha kuwa baadhi yao ni wale walioelimika na inasikitisha kuwa wao huvutiwa na pesa. Kweli, unajua wasichana wana mahitaji mengi,” akajibu
Mbunge wa Likoni Mishi Mboko alikerwa na kauli hiyo na kumshutumu Bi Cheptumo kwa kuonekana kutokuwa na uelewa mpana wa janga hilo.
Aidha, Wakenya kwenye mitandao ya kijamii walimshutumu Waziri huyo mteule, wengi wao wakisema hafai kupewa nafasi ya kuhudumu kama Waziri wa Jinsia.
Hata hivyo, Jumatano, wabunge wa mirengo yote miwili walipitisha ripoti ya Kamati ya Uteuzi, iliyoidhinisha uteuzi wa Bi Cheptumo.
Hata hivyo, baadhi yao, kama vile Julius Sunkuli (Kilgoris) walionekana kukerwa na kauli ya mjane huyo wa aliyekuwa Seneta wa Baringo marehemu William Cheptumo.
Lakini Bi Odhiambo (Mbunge wa Suba Kaskazini) alimtetea Bi Cheptumo huku akijitolea kumfundisha namna ya kushughulikia masuala muhimu ya umma.
“Bi Cheptumo hafai kulaumiwa kwani ni ulimi wake uliteleza. Mimi kama mtetezi sugu wa haki za watoto wa kike na wanawake nitamwelekeza kuhusu namna ya kushughulikia masuala kama hayo nyeti,” akaeleza.
Wabunge pia waliidhinisha uteuzi wa aliyekuwa Mbunge wa Mbeere Kaskazini Geoffrey Ruku kuwa Waziri wa Utumishi wa Umma.
Bi Cheptumo na Bw Ruku walipendekezwa na Rais William Ruto mnamo Machi 26, 2025, kuchukua nafasi za mawaziri wa zamani Aisha Jumwa na Justin Muturi, mtawalia.