Habari

Makao ya watoto 1,000 kutiwa kufuli serikali ikibuka na mpango mpya ‘bora zaidi’

Na KAMAU MAICHUHIE April 17th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

TAKRIBAN makao 1,000 ya watoto nchini yatafungwa kufuatia mpango wa serikali wa kuanzisha njia mbadala za kuwatunza watoto hawa wenye mahitaji maalum.

Serikali, kupitia Baraza la Kitaifa la Huduma za Watoto, imeanzisha mageuzi katika mfumo wa utunzaji wa watoto unaolenga kuanzisha utunzaji wa watoto katika jamii wala sio katika makao ya watoto.

Kwa miaka mingi, watoto mayatima na wengine waliotelekezwa na wazazi wao wamekuwa wakitunzwa katika makao ya watoto yaliyoko maeneo mbalimbali nchini.

Lakini sasa Afisa Mkuu Mtendaji wa Baraza la Kitaifa la Huduma za Watoto Adanoor Mohamed, kupitia taarifa, anatoa wito kwa wadau katika sekta hiyo kukumbatia mfumo huo mpya wa kutunza watoto.

Bw Mohamed alisema hatua hiyo itawasaidia kulainisha shughuli zao na kuelekeza rasilimali kwa utunzaji watoto katika mazingira ya familia na jamii.

“Utafiti umeonyesha kuwa utunzaji watoto katika makazi ya makao rasmi una madhara ya muda mrefu kwa watoto ilhali utunzaji wa kifamilia na kijamii unaleta manufaa makubwa,” Bw Mohamed akasema kwenye barua hiyo.

Barua hiyo imetumwa kwa makamishna wa kaunti, washirikishi wa watoto katika kanda, washirikishi wa masuala ya kijamii, maafisa wa huduma za watoto katika kaunti na wadau wengine katika sekta ya utunzaji watoto.

Kenya kwa kuzingatia mfumo wa kisheria wa kimataifa na kitaifa kuhusu utunzaji wa watoto, ilitayarisha Mkakati wa Kitaifa wa Utunzaji wa Watoto (2022-2032) unaotoa mwongozo kuhusu kuhamishwa kwa utunzaji wa watoto kutoka makao ya watoto hao hadi utunzaji katika mazingira ya kijamii.

Mkakati huo umejengwa katika mihimili mitatu inayojumuisha kuzuia utengano na kuboresha familia, njia mbadala za utunzaji kama vile utunzaji wa kinasaba na kuwalea watoto usiowazaa.

Pia unajumuisha ushirikishaji watoto katika utunzaji wa kifamilia na kijamii. Kulingana na takwimu za hivi punde kutoka idara husika ya serikali, kuna makao 902 ya watoto yanayositiri jumla ya watoto 44,070.

Aidha, kuna taasisi 30 za serikali zinazowahudumia watoto 1, 443. Mwaka jana, Serikali iliahidi katika Kongamano kuhusu Watoto la 2024, kutekeleza ajenda ya kimataifa ya kuondoa makao ya watoto.