Niliteleza ulimi, ajitetea waziri aliyesema wanawake huuawa kwa kufuata hela za waume
WAZIRI mpya wa Jinsia, Hannah Cheptumo, amewaomba msamaha Wakenya kwa matamshi yake yenye utata kuhusu visa vya mauaji ya wanawake alipokuwa akipigwa msasa na wabunge baada ya kuteuliwa kwa wadhifa huo.
Akihojiwa mbele ya Kamati ya Bunge la Kitaifa, Bi Cheptumo aliashiria kuwa wasichana wa vyuo vikuu wanaouawa kwenye vyumba vya kukodisha, aghalabu huwa kwenye harakati za kusaka hela.
Matamshi hayo yalivutia hisia kali miongoni mwa Wakenya kwenye mitandao ya kijamii huku baadhi wakitilia shaka ufaafu wa waziri mteule kuaminiwa majukumu ya kupiga kukabiliana na kero la mauaji ua wasichana na wanawake ambayo yamekithiri kote nchini.
Punde baada ya Bunge la Kitaifa kupitisha uteuzi wake Jumatano kama waziri mpya wa Jinsia, Sanaa, Urithi na Utamaduni, Bi Cheptumo aliwaomba radhi Wakenya kupitia mtandao wa kijamii wa X.
“Nilipokuwa nikihojiwa, nilitoa matamshi nikijibu swali kuhusu mauaji ya wanawake katika AirBnB. Ningependa kuchukua fursa hii kuwajibikia kauli hii na kufafanua msimamo wangu,” alisema Bi Cheptumo.
“Ninaomba radhi kwa dhati kwa matamshi haya. Siamini kuwa mwanamke yeyote (au binadamu yeyote) anastahili kuuawa katika hali yoyote.”
Kulingana naye, alikusudia “kueleza baadhi ya changamoto za kifedha zinazowakumba wanawake wengi lakini akaishia “kuhusisha kimakosa masuala mawili tofauti.”
Bi Cheptumo vilevile alisisitiza suala la mauaji ya wanawake limekithiri nchini na linapaswa kujumuishwa katika Katiba.
”Dhuluma kwa misingi ya kijinsia hujitokeza kote na katika kila pembe ya jamii na inaathiri wanawake wote licha ya uhalisia wao kijamii na kiuchumi,” alisema.
“Wanawake Wakenya wanastahili kulindwa katika na kwa hali zozote. Visa vya mauaji ya wanawake na aina nyingine za ubaguzi kwa misingi ya jinsia ni sharti vikabiliwe kwa uzito na kwa makini.”
“Nataka kila mama, baba na mtoto – kila Mkenya – ajue wanaweza kuniaminia kuwasilisha masuala haya kwa niaba yao kwa uwajibikaji,” alisema.
Bi Cheptumo ambaye ni wakili na mjane wake aliyekuwa Seneta wa Baringo, William Cheptumo, ni moja kati ya mawaziri wapya walioteuliwa na Rais William Ruto wanaosubiri kula kiapo cha afisi baada ya Bunge la Kitaifa kupitisha majina yao.
Akiwasilisha hoja ya kuwataka wabunge kupitisha uteuzi wa Bi Cheptumo na mbunge wa Mbeere Geoffrey Ruku kuwa waziri wa Utumishi wa Umma, Kiongozi wa Wengi, Kimani Ichung’wah alimtetea Bi Cheptumo akisema hajazoea kuangaziwa kitaifa.
“Tangu kisa hicho kilipotokea, nimezungumza naye (Cheptumo) na ameomba radhi kwa taifa, kamati ya teuzi, kwa bunge hili kwa matamshi hayo tatanishi na ninafikiri ni sawa tumuunge mkono binti huyu,” Ichung’wah alieleza wabunge.
“Pasipo kumtetea, ni sawa tuelewe hali ambamo mambo hayo yalisemwa. Mtu ambaye hajakuwa katika mazingira aliyokuwamo siku hiyo anaweza kufanya makosa madogo kama hayo.”
Hata hivyo, hii sio mara ya kwanza kwa mawaziri walioteuliwa na rais wamesababisha Wakenya kutilia shaka ufaafu wao kwa kushindwa kujibu au kujibu isivyofaa maswali yanayohusu majukumu yao mapya lakini hatimaye wote huishia kupitishwa na wabunge na kuanza kazi.