Habari

Mwanamume aambia korti jinsi kilimo cha bangi kina faida kuliko kile cha mahindi

Na TITUS OMINDE April 18th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

MWANAMUME mmojo wa umri wa makamo alishangaza mahakama ya Eldoret alipokiri kwamba anajihusisha na kilimo cha bangi kama mmea wa kitamaduni kwa ajili ya kuzalisha tiba za kiasili.

Kevin Tallam, 26, alimweleza hakimu mwandamizi Nancy Barasa kwamba amekuwa akipata riziki kutokana na biashara ya kilimo cha bangi na hakujutia kitendo chake kwani haoni makosa ya kupanda mmea huo ambao aliutaja kama malighafi ya dawa za tiba za kiasili.

“Nimekuwa nikijishughulisha na kilimo cha bangi kwenye kipande changu kidogo cha ardhi. Lengo langu kupitia kilimo hiki ni kuzalisha tiba za kiasili,” Bw Tallam aliambia mahakama.

Bw Tallam alisema amekuwa akipanda bangi katika shamba lake la robo eka ambapo alidai kuwa kilimo hicho kina faida kuliko kilimo cha mahindi.

Shtaka lilisema kuwa mnamo Aprili 13, 2025 katika Kijiji cha Kaptalanga, Kaunti ndogo ya Turbo alipatikana akiendeleza kilimo cha bangi ambayo ilikisiwa kuwa ya thamani ya Sh15,650.

Bw Tallam alikamatwa na maafisa wa polisi kutoka kituo cha polisi cha Baharini.

Mshtakiwa huyo alikamatwa kufuatia taarifa kutoka kwa mama mlezi.

Kwa mujibu wa polisi, zao hilo lilikuwa limekomaa tayari kuvunwa.

Mshtakiwa ambaye alikiri mashtaka atazuiliwa katika ruamande ya gereza la Eldoret akisubiri ripoti ya maafisa wa kurekebisha tabia.

Kesi hiyo itatajwa Aprili 29.

Miaka minne iliopita, Mbunge wa Dagoretti Kusini John Kiarie alifufua wito wa kubuniwa kwa sheria mabayo itahalalisha kilimo cha bangi kwa matumzi ya tiba za kiasili.

Bw Kiarie alidai kuwa kilimo hicho kina faida kubwa hivyo basi iwapo kitahalalishwa kitachangia pakubwa katika uchumi wa nchi.

Msimamo wa mbunge huyo uliungwa mkono na Seneta wa Narok Ledama Ole Kina ambaye alitilia maanani umuhimu wa kilimo hicho haswa kwa sekta ya afya.