Raia wa Haiti wakerwa na magenge, waandamana tena
PORT-au-PRINCE, HAITI
RAIA wa Haiti kwa mara nyingine waliandamana Jumatano wakitaka wahakikishiwe usalama dhidi ya majahili ambao wanaendelea kudhibiti taifa hilo wakipigania uongozi wa nchi.
Mvua kubwa ambayo ilikuwa ikinyesha haikuwazuia maelfu kujitokeza barabarani huku wakiteketeza magurudumu ya magari, wakiweka vizuizi barabarani na kupiga kemi kulalamikia kudorora kwa usalama.
Polisi wenye silaha walitazama tu raia hao wa Haiti wakiandamana. Hii ni kinyume na majuma mawili yaliyopita ambapo polisi walilazimika kutumia vitoza machozi kutibua maandamano ya maelfu ya raia.
Wakati huo, waliokuwa wakiandamana walikuwa wakitembea wakielekea afisi ya Alix Didier Fils-Aime ambaye Baraza la Uongozi wa Mpito Haiti, lilimchagua kuwa waziri mkuu Novemba mwaka uliopita.
Ghadhabu za raia wengi wa Haiti zimekuwa zikipanda kutokana na magenge kuendelea kudhibiti asilimia 85 ya jiji la Port-au-Prince ambalo zamani lilikuwa kisiwa cha amani.
Serikali ya Haiti mnamo Jumatatu ilitangaza kuwa ilikuwa imeidhinisha kile ilichorejelea kama ‘Bajeti ya Vita’ ya Sh35 milioni, pesa ambazo zitatumiwa kusaidia kuimarisha vita dhidi ya magenge.
Asilimia 40 ya pesa hizo zitaelekezwa katika kupiga jeki vikosi vya polisi na jeshi la Haiti kupambana na magenge yenye silaha ambayo yanatishia udhabiti wa taifa.
Asilimia 16 itaelekezwa kwenye miradi ya kijamii kama elimu, afya na misaada ya kibinadamu huku asilimia 20 ikitumiwa kudhibiti usalama na kulinda mpaka kati ya Haiti na Jamhuri ya Dominica.
Kwa kipindi cha mwezi mmoja uliopita, magenge yamechangia zaidi ya watu 60,000 kuhama makwao kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Umoja wa Kimataifa (UN) kuhusu uhamiaji.
Kuanzia Januari 1 hadi Machi 27, zaidi ya watu 1,500 wameuawa nchini Haiti huku wengine 572 wakijeruhiwa kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa. Umoja huo pia umebaini kwamba zaidi ya watu milioni moja hawana makao kutokana na uvamizi wa magenge hatari.