Habari za Kitaifa

Utafainiwa laki moja kwa kukataa malipo ya pesa taslimu

Na SAMWEL OWINO April 20th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

HUENDA wafanyabiashara, na watu binafsi, wakatozwa faini ya Sh100,000 ikiwa wabunge watapitisha mswada unaolenga kuhakikisha kuwa wale wasiotaka kulipia bidhaa na huduma kwa njia ya simu wanafanya hivyo kwa pesa taslimu.

Mswada wa Marekebisho ya Sheria ya Benki Kuu ya Kenya, 2025 unalenga kuhakikisha kuwa mfumo wa kulipia bidhaa kwa pesa taslimu unaendelea kukubalika, ikiwemo kulipia huduma za serikali.

“Mswada huo unahitaji biashara zinazouza bidhaa na huduma kwa watu binafsi sharti zikubali malipo ya pesa taslimu ya hadi Sh100,000. Vile vile, unaharamisha mtindo wa wafanyabiashara kuwatoza bei za juu wateja wanaohiari kulipa kwa pesa taslimu, na hivyo kuhakikisha uwepo wa usawa katika malipo,” mswada huo unasema.

Kulingana na mswada huo uliodhaminiwa na Mbunge wa Suba Kusini Caroli Omondi, idadi kubwa ya Wakenya bado wanalipia bidhaa kwa pesa taslimu ilhali baadhi ya watu wazee hawaelewi jinsi ya kulipia bidhaa kwa njia ya simu kama vile huduma ya M-Pesa.

Katika hali hiyo, watu kama hao huzuiwa kununua bidhaa wakiwa na pesa taslimu endapo wafanyabiashara watasisitiza kuwa sharti malipo yafanywe kwa njia ya simu, kielektroniki au kadi maalum za kulipia bidhaa.

Vilevile, Bw Omondi anasema idadi kubwa ya watu ambao hawana vifaa vya kisasa au intaneti inayohitajika kufanikisha malipo kwa njia ya kieletroniki au kadi maalum.

“Kwa kuhakikisha kuwa wafanyabiashara hawakatai pesa taslim au kuweka taratibu za malipo zinazobagua, mswada huu unalenga kulinda haki za watumiaji bidhaa na kuondoa ubaguzi kwa msingi wa mfumo wa malipo.”

Aidha, kwa kutoa mwongozo wa kisheria kuhusu kukubalika kwa malipo kwa pesa taslim, mswada huu unatoa uhakika wa kibiashara,” mswada huo unaeleza.

Hata hivyo, mswada huo unafafanua kuwa itakuwa ni lazima tu wa watu kutumia mfumo wa kulipia bidhaa kwa pesa taslim katika biashara zinazoonekana.

“Mtu anayevunja hitaji la sehemu hii, kando na kumfidia mteja mhusika, akipatikana na hatia atatozwa faini ya isiyozidi Sh100,000,” mswada huo unaeleza.

Mswada huo, ambao utasomwa kwa mara ya kwanza katika bunge la kitaifa, kabla ya wabunge kuanza likizo ndefu, unajiri wakati ambapo biashara zimebuni mienendo ya kukataa malipo kwa pesa taslim.