Mawakili, hakimu wamchangia pesa mjakazi aliyekuwa atupwe jela kwa deni la Sh18,223
YAYA aliyekodolewa macho na kifungo cha jela kwa kushindwa kulipa deni alilokopa la Sh18,223 alipata muujiza wake Alhamisi (Aprili 17, 2025) pale mawakili na hakimu walipomchangia pesa kuponyoka makali ya gerezani.
Ukumbi na kikao cha mahakama Milimani Nairobi uligeuzwa kuwa hafla ya kumchangia mshtakiwa huyo huku hakimu mkazi Justine Asiago anayeamua kesi za madeni madogo madogo akigeuka kuwa emcee (kiongozi wa mchango).
Mshtakiwa huyo aliyetambuliwa kwa jina Abigael alikuwa nusra asukumwe jela wakili Mark Omuga alipojitolea mhanga kumlipia deni hilo mshtakiwa.
Bw Omuga alieleza mahakama “nitamlipia mshtakiwa deni hili ijapokuwa mimi simjui.”
Wakili huyo alikuwa anasubiri kesi yake itajwe kupitia mtandao wa Microsoft Teams alipomsikia mshtakiwa akijitetea na kuomba mahakama imwonee huruma isimsukume jela.
Abigael alieleza mahakama anafanyakazi ya yaya na mshahara wake ni Sh5,000.
Alimweleza hakimu kwamba amesomea taaluma Fedha lakini hajafanikiwa kupata kazi. Pia aliomba mahakama imsaidie kupata kazi.
“Nitamlipia deni hilo,” Bw Omuga alimweleza hakimu.
Mawakili wengine pia ambao walikuwa wamefungua mtandao huo wakisubiri kesi zao zifikiwe walishiriki katika “harambee hiyo ya ghafla.”
Bw Omuga alieleza mahakama kuwa hamfahamu na hamjui Abigael na wala hajui jinsi mshtakiwa alivyokopa pesa lakini anastahili kusaidiwa.
Mshtakiwa alikuwa anaendelea na kesi akiwa na mtoto aliyeajiriwa kumtunza.
Mtoto huyo alikuwa anasikika anapiga kelele kesi ikiendelea.
Bw Omuga aliamriwa na hakimu awe mweka hazina wa mchango huo kisha naye awe emcee. Pesa zilitumwa kwa simu yake (Omuga).
Mawakili walituma kati ya Sh1,000 na Sh3,000.
Zaidi ya Sh22,000 zilichangishwa.
Wakili wa mlalamishi alitumiwa Sh18,233.
Pesa zilizosalia zilitumiwa Abigael kusherehekea siku kuu ya Pasaka.
Hakimu alimpongeza Bw Omuga anayefanya kazi katika kampuni ya mawakili ya Omuma Advocates LLP kwa kujitolea mhanga kumsaidia Abigael.
Bw Omuga alianza kazi ya uwakili 2016 baada ya kuhitimu kutoka chuo kikuu.
Bw Asiago alikuwa amemweleza mshtakiwa kwamba “hakuwa na budi ila kumfunga jela kwa kutolipa deni hilo.”
Mawakili na mahakama walipongeza mwito wa harambee wakisema “Hii ndio Kenya tunayoitaka ya kujali maslahi ya wengine.”
Abigael alimshukuru hakimu na kuwapongeza mawakili wote waliotoa mchango kumlipia deni.