Habari

Uchungu tele kwa waliofurushwa Mau huku mchezo wa ‘kujuana’ ukiingizwa kwenye fidia

Na FRIDAH OKACHI, TOBIAS MESSO April 21st, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MAELFU wa Wakenya waliofurushwa kutoka Msitu wa Mau mnamo 2019 bado wanasaka makao mbadala huku wengine wakiishi na marafiki au nyumba za kukodisha wakisubiri serikali iwape ardhi ya kujengea makao ya kudumu.

Hayo yanajiri huku madai ya ufisadi wakati wa kuteua watakaonufaika na fedha za fidia kutoka kwa serikali yakizuka.

Mwanaume  mmoja akiambia Taifa Leo kwamba alipokea pesa hizo siyo kwa sababu alipoteza makao bali alilipwa pesa hizo kama “asante” kutoka kwa mwanasiasa mwengine aliyemsaidia kushinda kiti.

Idadi ya waliopwa fidia ilikuwa ndogo, kwani wengi hawakupokea hata senti na wanapania kurejea katika msitu wa Mau.

Mhusika mmoja katika usajili wa watu waliolipwa fedha za fidia ni Jefferson Langat, diwani maalum katika Kaunti ya Narok.

Alikuwa mwanachama wa kamati iliyoendesha shughuli ya usajili wa waathiriwa wa shughuli ya kuwafurusha watu kutoka Msitu wa Mau.

Bw Langat aliambia Taifa Leo kwamba shughuli hiyo iliyoathiri zaidi ya watu 13,000 ilichochewa kisiasa.

“Nilizaliwa na kulelewa katika eneo linalojulikana kama Msitu wa Mau. Watu wengi walipoteza mali yao na wengi hawajalipwa fidia. Kati ya watu 13,500 waliofurushwa ni watu 2,000 pekee wamepewa makao mapya,” akasema Bw Langat.

Watu hao 2, 000 walitoka wadi za Ololunga, Malelo, Sogoo, na Segemian katika eneo bunge la Narok Kusini. Jamii za Ogiek na Kipsigis ndizo ziliishi maeneo hayo awali.

Walipewa makao mapya mnamo 2024 kutokana na hofu kutoka serikali za kitaifa na za kaunti kwamba mvua kubwa ingewaathiri wale waliokuwa wakiishi katika kambi za muda.

“Rais William Ruto alitenga Sh600 milioni….. Pesa hizi zilitumika kuwalipa fidia watu 2,000 katika kambi mbalimbali. Wengine waliosajiliwa katika awamu ya pili na awamu ya tatu hawajapokea chochote,” Bw Langat akaongeza.

Bi Zipporah Langat, ambaye ni mmoja wa wale walioishi katika kambi hizo za muda, aliambia Taifa Leo kwamba walipewa ilani ya miezi mitatu waondoke Msitu wa Mau.

“Baada ya miezi mitatu, maafisa wa polisi walifika na kutufurusha. Mimi na mume wangu tulikuwa tukijaribu kuondoa mahindi kutoka kwa ghala letu lakini nyumba yetu na ghala hilo ziliteketezwa,” Zipporah akaeleza.