Makala

Askofu Kivuva afokea Ruto kuhusu tamaa ya mikopo inayobebesha raia mzigo mzito

Na BRIAN OCHARO, STEPHEN ODUOR April 21st, 2025 Kusoma ni dakika: 3

ASKOFU Mkuu wa Mombasa, Martin Kivuva, amemuonya Rais William Ruto dhidi ya tamaa ya serikali yake ya kuchukua mikopo mingi, akisema taifa linazidi kulemewa na mzigo wa madeni ambao unaweza kuwa hatari kwa kizazi cha siku zijazo.

Katika ujumbe wake wa Pasaka, Askofu Kivuva alimhimiza Rais Ruto kuacha kukopa kupita kiasi na badala yake kutumia rasilimali chache zilizopo kwa uangalifu ili kukuza na kustawisha uchumi.

“Wakenya wanajiuliza: Je, mabilioni haya tunayokopa yanaelekezwa kweli kwenye miradi ya maendeleo? Pesa zinaenda wapi?” aliuliza, akifananisha hali ya Kenya na mtu anayezama kwenye madeni lakini bado anaendelea kukopa kutoka kila upande.

Alisema ingawa Rais anasisitiza kuwa anajua anachofanya, swali kuu ni nani atakayebeba mzigo huo baada ya kuondoka kwake madarakani.

“Sisi hatusemi kuwa Rais hajui—ameshaonywa hata na mataifa ya nje. Tunachotaka ni tahadhari kama taifa tusije tukaangamia,” alisema Askofu huyo, akiionya serikali dhidi ya kuendeleza ufisadi huku ikikopa pesa nyingi ambazo huweka hatarini mustakabali wa nchi.

Aliwahimiza Wakenya kuwa macho na kupaza sauti kila wanapoona mali ya umma ikihujumiwa au serikali ikichukua hatua zinazoweza kuhatarisha rasilimali za taifa, hasa iwapo kutatokea hali ya kutolipa madeni.

Katika Kaunti ya Tana River, viongozi wa kidini pia walitumia ibada ya Pasaka kukemea uongozi wa kitaifa na wa kaunti, wakihimiza waumini kusimama katika maombi na kukumbatia hekima.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kidini ya Wanaimani Mbalimbali, Mchungaji Robert Mkolwe, aliwalinganisha viongozi wa leo na Farao wa Biblia, akisema wanawakandamiza wananchi huku wakistarehe kwa jasho la walala hoi.

“Wanawaongezea watu ushuru, wanajenga majumba ya kifahari huku wananchi wakilala njaa. Mungu anaona, na atawalipiza kisasi,” alisema kwa msisitizo.

Aliwakemea wabunge waliopendekeza nyongeza ya mshahara kwa asilimia 50 huku wananchi wakilemewa na ushuru mzito, akisema hiyo ni dalili ya dhuluma na tamaa.

Kauli hiyo iliungwa mkono na Askofu Ethan Ndalo wa Kanisa la Faith, aliyewahimiza viongozi wa upinzani kuendelea kuwajibisha serikali, akisema upinzani ni wito wa Kiungu wa kutetea wanyonge.

Kwa upande wake, Askofu Kivuva alikemea siasa za mapema kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027, akisema wanasiasa wameanza kuwagawanya wananchi kwa misingi ya kikabila na kidini.

“Wameanza kupanga uchaguzi wa 2027 na kugawanya watu kwa misingi ya kikabila. Tunapaswa kulikataa hili na kuwakumbusha kuwa wao ni viongozi wa kitaifa,” alisema.

Alilaani pia wale wanaowahadaa vijana kuleta vurugu, akisema hiyo si njia ya kuleta amani, haki na maendeleo nchini.
Aliapa kuendelea kulaani ufisadi, akisema kiini chake ni ubinafsi.

“Tutasema kuhusu ufisadi kila wakati. Tamaa ya kutaka kumiliki kila kitu—ardhi, nyumba—kwa manufaa binafsi si ya umma, ndiyo chanzo,” alisema.

Aliwakumbusha wabunge na viongozi wengine kuwa wananchi wote walio katika maeneo yao ni sehemu ya wajibu wao, si majirani au wafuasi wao pekee.

“Tukifikiria kuhusu masikini, mabanda na watu wa kawaida, tutaepuka matatizo makubwa ya kijamii. Viongozi wasiwafikirie matajiri pekee,” aliongeza.

Aliwahimiza Wakenya kuishi kama familia moja na kusaidiana kukuza maisha ya kila mmoja.

Askofu huyo alisema wananchi wanafanya bidii lakini viongozi wanashindwa kutekeleza miradi yenye manufaa ya moja kwa moja kwao.

“Tukiungana na kusimama kidete dhidi ya uovu, tutajenga Kenya bora ambapo kila mmoja anajali mwingine,” alisema.

Alikumbusha serikali kurekebisha Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA) ili ihudumie Wakenya wote, hasa masikini, na kuchukua hatua za kupunguza gharama ya maisha.

Aliwaasa vijana kutokubali kutumiwa na wanasiasa kama vikundi vya uhalifu au kuzua vurugu.

“Nitarudia mara kwa mara: vijana msijitolee kuajiriwa na wanasiasa kwa fujo. Tuishi kwa amani na tushirikiane kuimarisha maisha yetu,” alisema.

Askofu Kivuva alitoa ujumbe huo wakati wa ibada ya asubuhi katika Kanisa Kuu la Holy Ghost, Mombasa, iliyohudhuriwa na mamia ya waumini.

Viongozi wa dini waliwahimiza Wakristo kote nchini kusali kwa ajili ya uongozi bora, umoja wa taifa lenye maadili wakati huu ambapo Kenya inakabiliwa na changamoto za kisiasa na kiuchumi.

Waliwahimiza raia kuwa waangalifu, wakatae siasa za kupotosha umma, na wakumbatie hekima katika kuwachagua viongozi wanaotamani kwa dhati taifa lenye ustawi, umoja, na maadili mema.