E-Citizen ni shimo hatari la kina kirefu, Wabunge sasa watoa kauli
WABUNGE wamebaini dosari kadhaa katika mkataba wa makubaliano kati ya kampuni za kibinafsi na serikali kuhusu uendeshaji na usimamizi wa mtandao wa kulipia huduma za serikali wa e-Citizen, kwani unaendeleza maslahi ya kibinafsi.
Kwa mujibu wa wabunge, kandarasi hiyo potovu inawaweka Wakenya katika hatari ya kupoteza kiasi kikubwa cha pesa na data muhimu.
Haya yamechipuza wakati ambapo Mkaguzi wa Hesabu za Serikali Nancy Gathungu anaendesha ukaguzi maalum kuhusu utendakazi wa E-Citizen baada ya malalamishi kuwa mtandao huo unasimamiwa visivyo.
Ripoti ya mkaguzi wa hesabu za serikali ya mwaka wa kifedha wa 2023/2024 inaonyesha kuwa jumla ya Sh44.8 bilioni zilipitishwa katika mfumo huo lakini ukaguzi wa akaunti hiyo ulionyesha kiasi tofauti cha pesa.
“Wakati huu, afisi hii inaendesha ukaguzi maalum wa jukwaa la kidijitali la E-Citizen. Ukaguzi huo unatokana na umuhimu wa E-Citizen katika shughuli za kulipia huduma za serikali. Ukaguzi huo maalum unatarajiwa kutoa mwanga kuhusu utendakazi wa E-Citizen ikiwemo hakikisho kuhusu iwapo data iliyotayarishwa kupitia mfumo huo ni sahihi na kamilifu.
“Hadi wakati ukaguzi huu ulipoanzishwa, ukaguzi maalum wa mfumo wa E-Citizen haukuwa umekamilishwa,” ripoti hiyo inaeleza.
Wabunge wanachama wa Kamati ya Bunge la Kitaifa kuhusu Usalama walimlaumu Katibu wa Wizara anayesimamia Idara ya Uhamiaji Belio Kipsang alipofeli kutoa habari sahihi kuhusu namna kandarasi ya uendeshaji wa E-Citizen ilivyojadiliwa na kutiwa saini.
Wabunge wanasema huku mamilioni ya pesa yakipitishwa katika mfumo huo kila siku, kandarasi ya usimamizi wake ilitiwa saini na afisa wa cheo cha chini, kuwakilisha serikali, na kampuni za kibinafsi kwa upande wa pili.
Wabunge walishangaa kuwa nakala za kandarasi hiyo zilizowasilishwa bungeni hazikuwa na saini ya Mwanasheria Mkuu ambaye ni mshauri mkuu wa serikali kuhusu masuala ya kisheria.
“Huwezi kutayarisha mkataba utakaotumiwa kupitisha matrilioni ya pesa bila kuwepo kwa saini ya Mwanasheria Mkuu, Waziri wa Fedha na Waziri wa Usalama wa Ndani. Hii inaibua hofu,” akasema mbunge mmoja mwanachama wa kamati, ambaye aliomba jina lake lisitajwe.
Mfumo wa E-Citizen unaendeshwa na kundi la kampuni za kibinafsi za kutoa huduma za kielektroniki. Kampuni hizo ni pamoja na Webmasters Kenya Limited, Pesaflow Limited na Olive Tree Limited.
Mbunge wa Kisumu Magharibi Rozza Buyu alimlaumu Dkt Kipsang’ kwa kuwasilisha stakabadhi hizo kwa kamati hiyo muda mfupi kabla ya mkutano huo.
“Tunafuatilia utendakazi wako kwa niaba ya raia. Wakenya wanataka kujua zinakoenda pesa wanazolipa,” akasema Bi Buyu.
Tangu mwaka jana, mtangulizi wa Dkt Kipsang, Julius Bitok, aliombwa na kamati hiyo awasilishe nakala za kandarasi hiyo lakini akafeli kufanya hivyo.
Huku kandarasi hiyo ikitarajiwa kudumu kwa miaka mitatu kutoka 2023 hadi 2026, haielezi tarehe kamili ya kuanza na kukamilika.
Sasa wabunge wanahofia kuwa dosari hiyo inaweza kutoa mwanya kwa pesa za umma kupunjwa.