Vatican ilivyotangaza kifo cha Baba Mtakatifu Francis aliyefahamika kwa mageuzi mengi
BABA Mtakatifu Francis, kiongozi wa kwanza wa Kanisa la Kikatoliki mwenye asili ya Amerika Kusini, ameaga dunia akiwa na umri wa miaka 88, Vatican imetangaza.
Kifo cha Papa kilitangazwa Jumatatu asubuhi na mweka hazina wa Vatican, Kadinali Kevin Farrell.
“Kaka na dada wapendwa, ni kwa huzuni kuu nimelazimika kutangaza kifo cha Baba Mtakatifu Francis wetu,” alisema mweka hazina kupitia taarifa.
“Asubuhi hii saa moja na dakika thelathini na tano Askofu wa Roma, Francis, alirejea katika nyumba ya Baba. Maisha yake yote yaliwekwa wakfu kuhudumia Mwenyezi Mungu na Kanisa Lake.”
Farrel alisema, “Alitufunza kuishi kuambatana na maadili ya Injili kwa uadilifu, ujasiri na upendo kwa wote duniani, hususan kwa kuwajali zaidi walio maskini na waliobaguliwa zaidi.”
“Tukiwa tumejawa na shukran kwa kielelezo chake kama mwanafunzi wa kweli wa Bwana Yesu, tumekabidhi roho ya Papa Francis kwa rehema na upendo unaodumu milele wa Mungu,” ilisema taarifa.

Tangu alipoteuliwa 2013, Baba Francis ambaye jina lake halisi ni Jorge Mario Bergoglio, alijidhihirisha kuwa mwanamageuzi.
Aliasi kanuni nyingi rasmi zinazohusishwa na mapapa wa awali huku akijitokeza kwa mara ya kwanza kwenye roshani ya kanisa la Kikatoliki la Saint Peter’s Basilica akiwa amevalia kasoksi nyeupe bila kofia nyekundu maarufu kama mozzetta, ambayo kwa kawaida ilivaliwa nyakati kama hizo.
Kifuani mwake alivalia msalaba wa fedha aliovalia alipokuwa askofu wa Buenos Aires, badala ya msalaba wa dhahabu uliovaliwa na mapapa waliomtangulia.
Vitendo vyake vya mwanzoni vilivyoonyesha mageuzi vilienda zaidi ya mavazi yake kwa sababu alikataa kuishi kwenye Kasri la Kiapostoliki, na badala yake kuishi kwenye nyumba ya wageni ya Domus Sanctae Marthae.
Mambo mengine aliyotanguliza ni pamoja na kujitwika jina Francis kwa heshima ya Saint Francis of Assisi, na kuwa papa wa kwanza aliyepatiwa jina la kipekee katika zaidi ya miaka 1,000 (wa mwisho akiwa Papa Lando mnamo 1913).
Sehemu kubwa ya mafunzo yake makuu almaarufu kama “barua za papa” ziliashiria hekima ya Saint Francis.
“Mizizi yangu ni Italia, lakini mimi ni mzaliwa wa Argentina na Amerika Kusini,” alisisitiza katika tawasifu yake ya hivi majuzi. Ni asili hii kama papa wa kwanza kutoka mwambao wa kusini na malezi yake nchini Argentina, iliyounda wajibu wake kama sauti ya waliotengwa katika jamii: wahamiaji, wachochole, wahasiriwa fukara wa vita na walalahoi.
Miezi michache kabla ya kifo chake, Papa aliyekuwa mtetezi sugu wa wahamiaji alishutumu vikali sera za rais wa Amerika Donald Trump kuhusu kuwarejesha kimabavu wahamiaji.
Uongozi wake uliokinzana na kuchipuka kwa utawala wa kitaifa, aghalabu umlimtia mashakani kutoka kwa viongozi wanajadi wenye nguvu wa Kikatoliki Amerika.
Kifo cha Francis, moja kati ya mapapa wakongwe zaidi katika historia ya Kikatoliki, kimetokea wiki kadhaa baada ya kuruhusiwa kutoka hospitali ya Roma alipopambana na maradhi sugu ya nimonia yaliyoathiri mapafu yote mawili.
Kifo chake kitaanzisha mdahalo mkali kuhusu mwelekeo wa Kanisa la Kikatoliki siku za usoni huku makadinali kutoka pembe zote duniani wakitarajiwa kukusanyika Roma siku zijazo kuwmomboleza papa na kumchagua mrithi wake.