Papa Francis alikuwa baunsa kilabuni kabla ya kuwa kasisi
PAPA Francis, ambaye alikufa Jumatatu, aliishi maisha ya uchochole, kabla ya kukumbatia ukasisi.
Kulingana na kumbukumbu kuhusu historia yake, Jorge Mario Bergoglio (alivyojulikana nchini mwake Argentina) alifanya kazi ndogo kujikimu na familia yake-ikiwemo kazi ya ulinzi kwenye vilabu vya burudani, almaarufu “bouncer”.
Aidha, aliwahi kufanyakazi katika kiwanda kimoja nchini Italia ambako babake, Mario Bergoglio alikuwa akifanyakazi kama mhasibu.
Akihutubu katika kanisa moja jijini Roma mnamo 2013, Papa Francis, aliyezaliwa Desemba 17, 1936, aliongeza kuwa aliwahi pia kufanyakazi ya kufagia katika kiwanda hicho cha kitengeneza kemikali za maabara na baadaye kuhudumu kama mwalimu wa shule ya upili.
Mnamo 1958, alivutiwa na kuwahudumia watu masikini na kujiendeleza kimasomo, alijiunga na kundi la kidini kwa jina Society of Jesus (Jesuits), ambalo lilifanyanga maisha yake ya kiroho.
Alianza kukumbwa na matatizo ya kiafya akiwa na umri wa miaka 20s ambapo alifanyiwa upasuaji wa kuondoa sehemu ya mapafu yake kutokana na maradhi hatari.
Hata hivyo, Raia huyo wa Argentina aliendelea na masomo yake ya kidini bila kufa moyo.
Alitawazwa kuwa kasisi mnamo 1969 na baadaye uongozi wake katika jamii ya Jesuit ilianza kutambuliwa.
Mnamo 1992, Papa John Paul II alimteuwa Bergoglio kuwa Askofu Msaidizi katika mji wa Buenos Aires nchini Argentina.
Alitawazwa mnamo Juni 27, mwaka huu baadaye mnamo 1997 akateuliwa kuwa Askofu Mkuu na akamrithi Kadinali Antonio Quarracino mnamo 1998 alipopandishwa cheo kuwa Kadinali.
Mnamo 2013, kufuatia kujiuzulu kwa Papa Benedict XVI, Bergoglio alichaguliwa kuwa Papa wa 266 na Kamati ya Makadinali akiwa na umri wa miaka 76.