Habari

Mpwa wa Raila ateuliwa mshauri wa Ruto

Na RUSHDIE OUDIA April 22nd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

RAIS William Ruto amemteua Jaoko Oburu, mpwa wa aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga, kuwa Mshauri wake kuhusu Uwezeshaji wa Kiuchumi na Maisha Endelevu.

Jaoko anatarajiwa kushikilia nafasi hiyo kwa kipindi cha miaka mitatu, na hivyo kujiunga na idadi inayozidi kuongezeka ya washauri wa Rais Ruto.

Uteuzi huo ulifanywa kupitia barua kutoka kwa Ofisi ya Mkuu wa Utumishi wa Umma na Mkuu wa Wafanyakazi wa Rais, Bw Felix Koskei, ambayo ilionekana na Taifa Leo.

“Nina furaha kukufahamisha kuhusu uamuzi wa Tume ya Huduma kwa Umma kwamba umeidhinishwa kuteuliwa kama Mshauri wa Uwezeshaji Kiuchumi na Maisha Endelevu, Daraja 2A,” inasema barua hiyo ya uteuzi.

Barua hiyo pia ilibainisha kuwa uteuzi huo ni kwa masharti ya ‘Mkataba wa Ndani’ na utadumu kwa kipindi cha miaka mitatu kulingana na muda wa uongozi wa Rais.

Kadi ya biashara yenye jina lake na wadhifa wake mpya imekuwa ikisambazwa katika mitandao ya kijamii tangu wiki iliyopita.

Jaoko alichapisha ujumbe kwenye mitandao ya kijamii kuthibitisha uteuzi huo.

Akikubali uteuzi huo, alimshukuru Rais Ruto kwa kumpa nafasi ya kuwahudumia Wakenya katika nafasi hiyo, na pia akamshukuru Bw Odinga kwa kumuamini na kwa kuunda mazingira mazuri kwa Wakenya wa kila tabaka kushirikiana katika ujenzi wa taifa.

‘Ninapochukua jukumu hili, nataka kuwahakikishia nyote kuwa uwezeshaji wa kiuchumi kwa maisha endelevu limekuwa jambo la moyoni mwangu kwa muda mrefu. Katika jukumu hili, najihisi kama samaki aliye majini. Naomba neema na msaada wa Mungu ili niweze kutekeleza kwa mafanikio jukumu hili muhimu kwa nchi yetu Kenya, na hata kwa bara la Afrika kwa ujumla,’ alisema Jaoko.

Aliwashukuru maelfu ya Wakenya, ndani na nje ya nchi, waliompongeza na kumpa moyo baada ya uteuzi wake kama Mshauri Maalum.

“Kwa wale waliowasiliana nami kuhusu masuala wanayotaka nishughulikie kwa haraka, ndani na nje ya jukumu langu, nawahakikishia kuwa nipo katika harakati za kuanzisha rasmi ofisi yangu na nitawasiliana nanyi hivi karibuni. Kwa sasa nawaomba subira, lakini nawahakikishia kuwa nitarudi kwenu,” alisema Bw Jaoko kwenye chapisho aliloambatisha picha yake akiwa na Rais Ruto.

Jaoko ni mvulana wa kwanza wa Seneta wa Siaya, Dkt Oburu Oginga.

Kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2022, aliacha nia ya kugombea kiti cha Ubunge wa Lang’ata ili kuelekeza nguvu zake kwenye kampeni za baba yake na mjomba wake, Bw Odinga.

Pia ilisemekana kuwa alikuwa na nia ya kugombea kiti cha Ubunge wa Bondo, ambacho baba yake alishikilia kwa zaidi ya miaka ishirini.

Hata hivyo, alijiondoa kwenye kinyang’anyiro hicho kwa sababu baba yake alikuwa akigombea kiti cha Useneta kaunti ya Siaya, baada ya kuwa Mbunge wa Bondo kwa mihula minne kuanzia 1994 hadi 2013, kabla ya kiti hicho kuchukuliwa na Dkt Gideon Ochanda ambaye kwa sasa anahudumu muhula wa tatu.

Badala yake, Jaoko alichukua jukumu la kuongoza vuguvugu la vijana lililojulikana kama “Young Turks Handshake Alliance” ambalo lililipigia debe Bw Odinga miongoni mwa vijana. Alisaidiana na kaka yake Elijah Oburu, ambaye alipoteza kwenye mchujo wa kiti cha Ubunge wa Kisumu ya Kati wa chama cha ODM.

Katika mahojiano ya awali na Taifa Leo alisema: “Bado hatujafika Canaan kama alivyotabiri babu yangu Jaramogi Oginga Odinga. Nina shauku kubwa kuhusu kile ninachofanya, na safari ya Jakom ambayo ilianza na Jaramogi, nataka tuiweke historia. Hadi tufanikishe hilo, siwezi kustarehe kufuatilia ndoto yangu binafsi kabla sijamsaidia mjomba wangu kuifikia ndoto hiyo.”

Jaoko, mwenye umri wa miaka 53, aliwahi kuwa waziri katika Kaunti ya Siaya akisimamia Barabara na Kazi za Umma chini ya Gavana wa zamani wa Siaya, Cornel Rasanga.