Karua: Ni wakati wa Kenya kuwa na rais mwanamke na niko tayari
KIONGOZI wa chama cha People’s Liberation Party (PLP), Martha Karua, ametangaza kuwa wakati umefika wa Kenya kuongozwa na rais mwanamke, akitoa wito kwa wananchi kumpa nafasi ya kuliongoza taifa katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kaunti ya Isiolo, Karua alisema kuwa wakati umefika kwa wanawake kupewa fursa ya kuleta mabadiliko ya maana nchini. Alitoa mfano wa mama anavyojitahidi kutunza familia yote bila kubagua mtoto yeyote.
“Mungu akinijalia, kile kiti mimi nawania ni cha urais,” Karua alieleza.
“Ili kama mama niweze kutunza Kenya kama vile mama anatunza boma. Mama hawezi kuacha mtoto hata mmoja kulala njaa, hata chakula ikiwa kidogo anagawa kidogo kidogo kisha kila mtu anapata.”
Kulinganana Karua, mapato ya taifa yanapaswa kugawa kwa usawa, tofauti na jinsi inavyogawa kwa sasa. Alisema kuwa kwa muda mrefu taifa limekuwa likiwaamini wanaume, lakini sasa ni wakati wa kujaribu uongozi wa mwanamke.
“Mumejaribu wanaume siku hizo zote, tafadhali wakati huu jaribuni mama wa PLP,” alisema huku akishangiliwa na wafuasi wake.
Karua ameonekana kushirikiana kwa karibu na viongozi wengine wa upinzani kama Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, Naibu Rais wa zamani Rigathi Gachagua, na Kiongozi wa DAP-K Eugene Wamalwa, katika juhudi za kuunganisha nguvu dhidi ya utawala wa Kenya Kwanza.
Upinzani umeapa kuungana ili kuondoa serikali ya Kenya Kwanza madarakani katika uchaguzi wa 2027.
Tangu Kenya ipate uhuru mwaka 1963, haijawahi kuongozwa na rais mwanamke. Ingawa wanawake kadhaa wamewahi kuwania nafasi hiyo, hawajawahi kushinda.
Mbali na Karua, Mbunge wa Githunguri, Gathoni Wamuchomba, pia ameeleza nia ya kuwania kiti cha juu zaidi nchini.
Ingawa hajathibitisha moja kwa moja kama atawania mwaka 2027, amekuwa akiashiria kuwa na ndoto kubwa akieleza maono makubwa ya kuleta mageuzi katika uchumi na sekta mbalimbali za maendeleo.