Kiazi moto: Sudan yaandikia Bunge la Kenya ikihusisha Ruto na ghasia nchini humo
AFISA mmoja wa cheo cha juu katika bunge la Kenya amethibitisha kupokea barua ya malalamishi kutoka kwa serikali ya Sudan, iliyomhusisha Rais wa Kenya William Ruto miongoni mwa wanaohusika na machafuko nchini Sudan kutokana na msaada wake kwa kikosi cha RSF, ambacho kinatuhumiwa kwa kutekeleza uhalifu nchini humo.
Hata hivyo, afisa huyo hakutaka kutoa taarifa rasmi, akisema “suala hili ni kiazi moto na litashughulikiwa katika ngazi za juu.”
“Barua hii itapitia njia za kawaida serikalini kupitia Wizara ya Masuala ya Nje,” alisema afisa huyo akiongeza, “wabunge wametahadharishwa dhidi ya kutoa maoni kuhusu suala hili.”
Barua hiyo iliyoandikwa Machi 14, 2025, kutoka kwa Makamu wa Rais wa Baraza la Mpito la Utawala la Sudan (TSC) Kamanda Malik Agar, pia inaomba wabunge wa Kenya kushinikiza Rais Ruto aondoe viongozi wa RSF nchini Kenya na kuepuka kuingilia masuala ya ndani ya Sudan.
RSF inaongozwa na Mohamad Hamdan Dagalo maarufu kama Hemedti.
Barua ya Agar inajiri wakati uhusiano kati ya nchi hizo mbili, ambazo hapo awali zilikuwa majirani kabla ya Sudan Kusini kujitenga na Khartoum, umekuwa baridi kabisa.
Sudan imekosoa Kenya kwa kusaidia kuchochea vurugu nchini Sudan, jambo lililosababisha Sudan kupiga marufuku bidhaa kutoka Kenya—hasa chai na kahawa ya Kenya, jambo linaloathiri chanzo kikuu cha mapato cha taifa la Kenya.
“Natumai kwamba Bunge lenu la heshima litahifadhi urithi wa Uafrika na halitaruhusu ardhi ya Kenya kutumika kuhalalisha au kuandaa vyombo vinavyolenga kudhoofisha utawala wa taifa jirani la Afrika,” alisema Agar.
Hii ni pamoja na kwamba Agar alieleza masikitiko ya Sudan kuhusu matukio ya hivi karibuni ambayo yanahatarisha misingi ya umoja na ushirikiano kati ya mataifa ya Afrika.”
Ombi lake kwa bunge la Kenya linajiri baada ya ombi sawa kwa Rais Ruto kuhusu kuendelea kwa Kenya kuwa mwenyeji wa viongozi wa RSF.
“Kulingana na barua yangu ya awali kwa Rais William Kipchirchir Samoei Arap Ruto, ninataka kuonyesha umuhimu wa uhusiano wetu wa muda mrefu na wa kindugu na Jamhuri ya Kenya, ambao umejengwa kwa heshima ya pande zote, mapambano ya pamoja, na maono ya pamoja ya Afrika yenye amani na ustawi,” alisema Agar.
Makamu wa Rais wa TSC alikumbusha wabunge wa Kenya kwamba Afrika imepiga hatua kubwa kutoka kwa enzi za ukoloni na ubaguzi wa rangi.
Huku serikali ya Sudan ikikashifu viongozi wa Kenya kwa kuwa na biashara fiche na kiongozi wa RSF na kusaidia waasi wanaopigana na serikali, imekataa jukumu la Kenya katika kupatanisha pande zinazopigana vita vya wenyewe kwa wenyewe Sudan.