Habari za Kitaifa

Majangili watawala barabara Baringo

Na FLORAH KOECH April 24th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WIMBI jipya la mashambulizi ya majangili limekumba barabara kuu za Kaunti ya Baringo, ambapo majambazi sasa hawalengi tena mifugo pekee, bali wameanza kuiba kwa nguvu kutoka kwa wafanyabiashara na watumiaji wa barabara mchana peupe.

Katika tukio la hivi punde, watu wawili waliuawa na mwingine kujeruhiwa baada ya genge la watu wenye silaha kuvamia msafara wa malori uliokuwa ukielekea Chemolingot, Tiaty Magharibi, Jumatatu asubuhi. Msafara huo wa magari 15 ulikuwa ukisafirisha bidhaa na wafanyabiashara kutoka Mogotio na Marigat kuelekea soko la mifugo la Nginyang.

Shambulizi hilo lilifanyika saa mbili na nusu asubuhi katika eneo la Loberer, dakika 15 tu baada ya msafara kuondoka Marigat, licha ya kuwepo kwa ulinzi wa polisi. Majangili walifyatulia risasi magari hayo, kuiba mali, na kutorokea kichakani.

“Dereva wa lori moja alikimbia porini kwa hofu, lakini wahalifu walimfuata na kumpiga risasi hadi kufa,” alisema Johnstone Kiprich, mmoja wa wafanyabiashara waliokuwa kwenye msafara. Mfanyabiashara mwingine alipigwa risasi na kufariki alipokuwa akipokea matibabu katika Hospitali ya Marigat.

Dereva mwingine, Joseph Ng’ang’a, alinusurika baada ya risasi kupita karibu na sehemu aliyokuwa ameketi. “Niliharakisha gari kuokoa maisha yangu, lakini mfanyabiashara aliyekuwa kando yangu alipigwa risasi na kufa papo hapo,” alisema.

Wakazi na wafanyabiashara sasa wanasema kuwa barabara tatu za Loruk–Chemolingot, Loruk–Kagir, Yatya–Chemoe, na Ng’aratuko–Kagir zimekuwa hatari, huku majambazi wakijificha vichakani wakiwasubiri wasafiri.

Bi Agnes Tepkeny, mfanyabiashara mjini Marigat, alisema hali hiyo imezua hofu kubwa. “Huu si tena wizi wa mifugo bali ni mtandao wa wahalifu wanaolenga biashara na magari ya abiria. Serikali inapaswa kuongeza doria haraka,” alionya.

Kamishna wa Kaunti ya Baringo, Bw Stephen Kutwa, alithibitisha tukio la Jumatatu na kueleza kuwa serikali imeanza kutoa ulinzi wa polisi kwa wasafiri wote katika barabara hatari. “Kwa masikitiko, tumepoteza watu wawili na mmoja amejeruhiwa. Tunafuatilia wahalifu hao na tutawafikisha mahakamani,” alisema.

Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Baringo, Julius Kiragu, alisema kuwa mbinu za majangili sasa zimebadilika. “Hili si suala la ujangili wa kawaida tena, bali ni uporaji wa barabarani unaofanywa na vijana.Tumeimarisha doria na kuahidi usalama kwa wakazi,” alisema.

Wakazi wa vijiji vya Kosile, Yatya, Ng’aratuko, Kagir, Chemoe, Chepkesin, na Natan sasa wanaishi kwa hofu kubwa. Wanaripoti kuwa hawawezi kuendesha shughuli za kila siku kwa amani kutokana na majangili waliojihami wanaoua bila huruma.