Uncategorized

Kaunti yakanusha madai ilihamisha Sh2.2 bilioni za madeni

Na  STANLEY NGOTHO April 24th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

Serikali ya Kaunti ya Kajiado imekanusha madai kuwa Sh2.2 bilioni  zilizotengwa kwa ajili ya kulipa madeni zilielekezwa kwa matumizi mengine.

Waziri wa Fedha na Mipango ya Kiuchumi wa Kaunti hiyo, Alais Kisota, sasa anasema kuwa kiasi hicho kilikuwa ni pengo la mapato yaliyotarajiwa katika bajeti ya mwaka wa fedha 2023/2024.

Katika rekodi mbalimbali za kifedha alizowasilisha, Kisota alieleza kuwa kaunti ilitarajia kupokea jumla ya Sh11.5 bilioni 11.5, ambapo Sh 8 bilioni zilitoka kwa Hazina Kuu, Sh 2 bilioni zikiwa ni ruzuku maalum na Sh 1.5 bilioni zikikusanywa kama mapato ya ndani ya kaunti.

“Hata hivyo, Kaunti ilipokea Sh 7.6 bilioni kutoka Hazina Kuu, Sh 456 milioni kutoka kwa ruzuku, na kukusanya mapato ya ndani ya Sh 1.1 bilioni.  Hii  ni jumula ya Sh 9.2 bilioni dhidi ya matarajio ya Sh 11.5 bilioni, hivyo kuleta pengo la Sh 2.2 bilioni,” alisema Kisota katika taarifa kwa vyombo vya habari.

Waziri huyo pia aliongeza:”Kuna upotoshaji wa makusudi unaoenezwa na chombo fulani cha habari kwa malengo ya kisiasa ya ndani. Mtu angehitaji tu kuelewa takwimu au hata kusoma nyaraka zinazotajwa ipasavyo.”

Kisota alisema haiwezekani kabisa kwa kiasi kikubwa cha fedha kama hicho kilichotengwa kulipa madeni muhimu kuhamishwa kwa matumizi mengine:
“Kwa kweli, katika bajeti zote zilizopitishwa na Bunge la Kaunti ya Kajiado, kiwango cha juu zaidi cha fedha zilizowahi kutengwa kwa  madeni ni takriban Sh 1 bilioni. Kwa hivyo hata kufikiria kuwa Sh 2 bilioni zingeweza kuhamishwa ni propaganda tu ya kisiasa.”

Aliongeza kuwa kaunti inafuata taratibu thabiti za usimamizi wa fedha:
“Tuko mbioni kulipa madeni yaliyosalia ili kuhakikisha kuwa miradi yote iliyoanzishwa inakamilika. Hata hivyo, pengo la mapato la Sh 2.2 bilioni linaathiri si tu ulipaji wa madeni hayo, bali pia linazidisha tatizo la madeni.”

Kisota alisisitiza:”Kwa hivyo, ni kwa nia mbaya tu mtu kudai kuwa fedha hizi za kulipia madeni zinaweza kuelekezwa kwenye matumizi mengine. Ukosefu wa fedha za kulipa madeni yaliyoidhinishwa mwishoni mwa mwaka husababisha kuhamishiwa kwa madeni hayo hadi mwaka unaofuata.”

Alitoa stakabadhi zinazoonyesha kuwa kaunti tayari imelipa madeni ya Sh570 milioni katika miezi tisa ya kwanza ya mwaka huu wa kifedha.
“Hii ni dhidi ya bajeti ya madeni ya Sh 958 milioni kwa mwaka unaoishia Juni 30, 2025,” alisema Kisota.