Serikali sasa kutumia sheria ya siri kuzima domo Gachagua na Muturi
SERIKALI imeanza kutumia Sheria ya Siri za Serikali ili kuzima kuanikwa kwa taarifa za ndani zinazolenga kufichua maovu serikalini, hatua ambayo inachukuliwa kama njia ya kulenga aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua na aliyekuwa Waziri wa Utumishi wa Umma Justin Muturi.
Waziri wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen, alipokuwa mbele ya Kamati ya Bunge kuhusu Utawala na Masuala ya Ndani, alitahadharisha kuwa wale wanaoanika taarifa za “siri za serikali” watachukuliwa hatua kali kwa mujibu wa sheria hiyo.
“Kuna watu walio wakubwa kiumri lakini hawaheshimu sheria hii. Ni hatari kubwa kwa nchi,” alisema Murkomen.
Kifungu cha 3 cha sheria hiyo kwa kusomwa pamoja na kifungu cha 20, kinasema mtu yeyote anayeshikilia au kupewa taarifa ya serikali kwa siri na akaisambaza, anavunja sheria na anaweza kufungwa jela hadi miaka 14 bila faini.
Lakini kauli hiyo ilipingwa vikali na Justin Muturi, pamoja na mawakili David Ochami na Anthony Musau, waliotaja hatua hiyo kuwa kinyume na Katiba, hasa haki ya kujieleza na kutoa maoni.
Muturi, ambaye aliwahi kuwa Mwanasheria Mkuu wakati mwanawe alitekwa nyara alisema alishinikizwa na Rais William Ruto kutia saini mkataba wa mabilioni ya pesa za mpango wa upanzi wa miti akiwa uwanja wa ndege nje ya nchi.
“Rais alinitimua hadharani, nami nikamjibu. Siwezi kujibizana na Murkomen kwa sababu sio wa kiwango changu,” alisema Muturi.
Rigathi Gachagua naye amekuwa akifichua biashara kati ya Rais Ruto na viongozi wa kundi la Rapid Support Forces (RSF) linalohusishwa na mzozo wa kisiasa nchini Sudan.
Wakili Ochami alisema sheria hii haifai kuzuia ufichuzi wa maovu au uhalifu serikalini, hasa ikiwa taarifa hiyo inalinda maslahi ya umma.
“Sheria ya Siri haipaswi kuwa kizuizi cha haki ya kujieleza. Katiba inaruhusu kuzimwa kwa maoni tu ikiwa yanachochea vita au chuki.”
Wakili Musau alisema sheria hiyo inakiuka maadili ya kidemokrasia.
“Kinachotia hofu zaidi ni matumizi yake na serikali kupuuza maadili ya katiba yetu.Katiba ndiyo sheria kuu ya nchi.”