Matumaini wasichana 1, 544 wasiojiweza wakipata ufadhili wa karo
NDOTO ya Michelle Omondi ya kumaliza masomo yake upili katika Shule ya Wasichana ya Pangani nusura ikatizwe kutokana na ukosefu wa karo.
Michelle, 15 anatoka familia maskini lakini sasa anaweza kufurahi baada ya shirika moja lisilo la kiserikali kumsaidia na kumpa udhamini wa masomo.
Tineja huyo ni kati ya wasichana na wanawake 1, 544 ambao SHOFCO imewalipia karo ili wamalize masomo ya shule ya upili katika Kaunti ya Nairobi.
“Kuna wakati ambapo nilifikiria ningeacha masomo na kuanza kusaka vibarua vya kusaidia familia yangu. Kulipiwa karo kumenisaidia sana na kunipa matumaini ya kusaka maisha bora,” akasema Michelle.
Bi Maureen Isinga, mzazi katika Shule ya Wasichana ya Huruma, naye alisema mwanawe alikuwa na deni la karo lakini sasa anaweza kutabasamu baada ya Shofco kumlipia deni hilo na kugharimia elimu yake yote.
“Hawajamlipia tu karo, pia wamelipa deni la awali ambalo lilikuwa likinisumbua. Sasa nitamakinika kusaka karo kwa watoto wangu wawili,” akasema Bi Isinga wakati Shofco ilizindua utoaji udhamini wa karo Nairobi.
Wanafunzi kutoka kaunti mbalimbali ndogo ambao wanatoka familia maskini na ni werevu walinufaika kwa kulipiwa karo.
Wakati wa hafla hiyo, Afisa Mkuu Mtendaji wa Shofco , Bw Kennedy Odede, alisema shirika hilo lina imani kuwa kupitia elimu, maisha ya familia nyingi maskini yataimarika.
“Elimu inastahili kuwa haki na wasichana hawa wameonyesha ari na bidii masomoni licha ya kutatizwa na karo. Tunawekeza kwenye taaluma yao ya baadaye kupitia ufadhili huu ambao tunawapa,” akasema Bw Odede.
Kati ya 1, 544 walionufaika, 159 walikuwa wasichana waliojifungua watoto na wamerejelea masomo ili kutimiza ndoto zao za kupata elimu.
Shofco inalenga kuwasaidia zaidi ya wasichana 11,000 maskini kwa kuwapa udhamini wa masomo kote nchini.