Jamvi La Siasa

Murkomen atatizwa na ushawishi wa Kalonzo akiwa ziara ya siku tatu Ukambani

Na PIUS MAUNDU April 28th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

USHAWISHI wa Kiongozi wa chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka ulimtatiza Waziri wa Usalama wa Ndani, Kipchumba Murkomen, alipozuru eneo la Ukambani kwa siku tatu ili kukusanya maoni kuhusu jinsi ya kuboresha usalama.

Kilichovumishwa zaidi kama mikutano ya mashauriano kuhusu usalama kwa jina ‘Jukwaa la Usalama’ kiligeuka kuwa wito wa kushirikiana kwa karibu zaidi kati ya wananchi, idara za usalama na serikali ili kudhibiti mizozo ya ardhi, matumizi ya dawa za kulevya, ukatili wa kijinsia, unyang’anyi barabarani na uharibifu wa miundombinu muhimu, masuala ambayo yaliibuka kama changamoto kuu za usalama katika kaunti za Kitui, Machakos na Makueni.

Hata hivyo, Bw Murkomen alijikuta akikabiliana na ushawishi wa kisiasa wa Bw Musyoka katika eneo hilo, huku wandani wa aliyekuwa Makamu wa Rais wakitumia majukwaa hayo kuthibitisha kuwa bado ana ushawishi mkubwa katika ngome yake ya kisiasa.

“Mwambieni Bw Musyoka ajiunge na serikali jumuishi sasa. Kwa nini aendelee kubahatisha kamari katika siku za usoni? Tunaweza kushirikiana kama Wakenya leo tunapopanga uchaguzi wa kesho,” Bw Murkomen alisema alipokamilisha ziara yake Ukambani mjini Machakos, Jumamosi.

Waziri huyo alikuwa akijibu kauli ya Naibu Gavana wa Machakos, Francis Mwangangi, ambaye alimwambia ajiandae kwa urais wa Bw Musyoka.

Bw Mwangangi ni miongoni mwa viongozi wa kisiasa wa Ukambani waliochukulia ziara ya Bw Murkomen katika Kaunti za Kitui, Machakos na Makueni kama maandalizi ya ziara ya Rais William Ruto katika eneo hilo.

Akitoa kauli kama ile ya Seneta wa Makueni, Daniel Maanzo, wakati wa mkutano wa Jukwaa la Usalama katika mji wa Wote, Bw Mwangangi alisema Rais Ruto hana nafasi ya kushinda kura za Ukambani.

“Tuna kiongozi wetu wa kisiasa hapa ambaye tuko waaminifu kwake. Akituambia twende kulia, tunaenda kulia. Akisema kushoto, tunaenda kushoto. Msidanganywe. Mwambieni Rais Ruto kuwa njia pekee ya kuingia Ukambani ni kupitia kwa Bw Musyoka,” Bw Mwangangi alimwambia Bw Murkomen.

Bw Murkomen na Katibu Mkuu wa Usalama wa Ndani, Raymond Omollo, waliwaongoza maafisa wa usalama kuweka msingi wa mapambano mapya kati ya Rais Ruto na Bw Musyoka kuhusu mizozo ya ardhi inayozidi kuongezeka katika Kaunti ya Machakos, baada ya suala hilo kufikishwa katika Baraza la Usalama la Kitaifa.

Akitaja ardhi kama tishio kubwa zaidi kwa usalama Machakos, Bw Murkomen aliwataja wanasiasa mashuhuri, wafanyabiashara na maafisa wa serikali kuwa miongoni mwa genge la ulaghai linalonyakua ardhi ya umma na ya kibinafsi katika kaunti hiyo.

“Wengi wa wanyakuzi wanaotusumbua Machakos wamenunuliwa, kusafirishwa na kulipwa ili kuvamia ardhi ya watu binafsi na ya umma kwa nia ya kuimiliki baadaye. Haya ni magenge yaliyokodishwa kutoka maeneo mbalimbali ya nchi na genge la wanyakuzi wa ardhi. Tumeweza kuwaondoa wavamizi kutoka ardhi ya kampuni ya East African Portland Cement huko Mavoko, lakini tatizo bado lipo,” Bw Murkomen aliwaambia waandishi wa habari mjini Machakos.

“Tumeamua kwa mujibu wa taarifa za kiusalama tulizopokea leo kuwa suala hili lifikishwe kwenye Baraza la Kitaifa la Kijasusi, na kwamba lazima tuwe na mkakati pamoja wa kukabiliana na udanganyifu wa umiliki wa ardhi Machakos, bila kujali serikali iliyoko madarakani,” alisema.

Matokeo ya hatua hii ni kuwa Rais Ruto, ambaye ndiye mwenyekiti wa Baraza la Usalama la Kitaifa, atakuwa na jukumu kubwa zaidi katika kukabiliana na wanyakuzi wa ardhi katika Kaunti ya Machakos, jambo ambalo litazua mvutano mkali na Bw Musyoka ambaye amekuwa mtetezi wa haki za wakazi wanaodai kumiliki baadhi ya ardhi inayozozaniwa sehemu kadhaa za Machakos.