Uchanganuzi: Ruto anachimbia Kenya shimo kubwa kwa kukopa
IFIKAPO jioni leo, Kenya itakuwa imetumia Sh5.1 bilioni kulipa madeni. Hali hii itajirudia kesho, keshokutwa, na siku inayofuata. Katika mwaka huu wa fedha, taifa litatumia jumla ya Sh1.866 trilioni kulipa madeni, hii ni sawa na Sh5.1 bilioni kwa siku.
Kwa muktadha, Wizara ya Afya imetumia Sh127 bilioni tu mwaka huu. Hii ina maana kuwa pesa zinazolipwa kwa madeni kila siku zinaweza kufadhili wizara hiyo kwa wiki mbili.
Kwa sasa, deni la taifa limefikia Sh11.02 trilioni.
Kwa Rais William Ruto, ambaye amerudi kutoka China na ahadi mpya za misaada ya kiuchumi, ikiwa ni pamoja na kuendeleza reli ya kisasa (SGR) hadi Malaba, mambo ni mazito.
Bajeti yake ya mwisho ilikataliwa na umma uliojawa na hasira.
Sasa, huku madeni yakiiva, wananchi wanalilia huduma, na mpango mpya wa IMF ukitazamiwa, Rais Ruto anakabiliana na changamoto kubwa ya kisiasa na kiuchumi ambayo inaweza kufafanua urais wake na mustakabali wa Kenya.
Wakati Mwai Kibaki alipoondoka madarakani mwaka 2013, Kenya ilikuwa inadaiwa Sh1.894 trilioni, sawa na asilimia 51.7 ya Pato la Taifa (GDP). Alikopa kwa kiasi na akawekeza kwenye barabara kama Thika Superhighway. Kiasi kilicholipwa kwa madeni kwa siku kilikuwa Sh400 milioni,
Kiwango kinachoweza kulipwa bila tatizo.
Lakini Uhuru Kenyatta alipoingia, mambo yalibadilika. Katika miaka yake 10, alikopa Sh6.7 trilioni, karibu mara tano alizokopa Kibaki.
Kufikia 2022, Kenya ilitumia Sh2.1 bilioni kulipa deni kila siku.
Sasa chini ya Rais Ruto, kiasi hicho kimefika Sh3 bilioni kwa siku, huku thamani ya shilingi ikizidi kushuka.
Reli ya kisasa ya SGR, iliyoanzishwa mwaka 2014 kwa mkopo wa Sh327 bilioni kutoka China, ilikuwa ndoto ya kuunganisha Afrika Mashariki.
Lakini mwaka 2018, Uganda ilijiondoa kutokana na kucheleweshwa kwa Kenya.
Sasa, reli hiyo inagharimu Sh56.85 bilioni kila mwaka kuiendesha, jambo ambalo mwanauchumi Kwame Owino anaita ‘ matumaini yasiyotimia.’
“Kenya ilipaswa kudhibiti mikopo mapema. Badala yake, SGR imebaki kuwa kumbukumbu ya matumaini yasiyotimia,” alisema Owino.
Mwaka 2014, Kenya ilikusanya Sh280 bilioni kwa Eurobond ya kwanza. Lakini Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali Edward Ouko alipata kuwa fedha hizo hazikuweza kufuatiliwa, ziliingia akaunti kuu ya serikali bila maelezo ya miradi iliyofadhiliwa.
“Fedha zilipokelewa lakini haziwezi kuhusishwa moja kwa moja na mradi wowote,” alisema Ouko katika ripoti yake.
Mnamo mwaka 2019, Kenya iliwasilisha tena Eurobond Sh271.7 bilioni kufadhili miradi yake ya miundombinu. Hata hivyo, kufikia mwaka 2024, nchi ilikumbwa na hofu ya kushindwa kulipa madeni yake, na hivyo kulazimika kununua Sh324 bilioni za bondi hizi. Ili kufadhili ununuzi huu, Kenya ililazimika kukopa tena, na kuunda mzunguko wa kukopa ili kulipa madeni. Hali hii inajulikana kama ‘kumuibia Petero ili kumlipa Paulo.’
Kati ya 2013 na 2022, Sh11 bilioni zilipotea kupitia kashfa kama ile ya Huduma ya Vijana (NYS). Kwame Owino asema: “Deni kubwa linatokana na mikopo na ufisadi wa zamani.”
Mwaka 2024, IMF ilikosea makadirio ya deni la Kenya kwa kusema ni asilimia 73 ya GDP, wakati ilikuwa asilimia 65.6. Hii ilisababisha masharti makali ya ushuru, ambayo yalisababisha maandamano makubwa ya Gen-Z.
“Makosa ya IMF yangeepukwa, huenda maisha yasingepotea,” Owino alisema
Rais Ruto aliporudi kutoka China, alitangaza msaada wa Sh194.2 bilioni kwa miradi ya miundombinu, ikiwa ni pamoja na kuendeleza SGR hadi Uganda. Wawekezaji wa China pia waliahidi mabilioni kwa viwanda vya nguo na vifaa vya elektroniki.
Lakini hata msaada huu una masharti na mzigo mpya wa deni. Rais Ruto analazimika kuahidi kuwa atakopa kwa busara.
Waziri wa Fedha John Mbadi ameahidi kutotoza kodi mpya kubwa kwa wananchi waliokandamizwa na hali ngumu ya kiuchumi.
“Hatuna chaguo lingine, lazima tuwe waangalifu. Hakuna uchumi unaokua bila kukopa,” alisema Mbadi.
Lakini ikiwa na deni la Sh11 trilioni, ukweli ni kwamba Kenya inalipa gharama ya kila siku si tu kifedha, bali pia kisiasa.