Siasa

Jamii ya Abagusii yampa Jalang’o saa 48 kufuta madai kwamba wao ni ‘wachawi’

Na RICHARD MUNGUTI April 29th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

JAMII ya Abagusii kupitia mawakili Danstan Omari na Samson Nyaberi imempa Mbunge wa Lang’ata Phelix Odiwuor Khodhe almaarufu Jalang’o masaa 48 kufutilia mbali matamshi kwamba ni “wachawi”.

Katika barua iliyopelekewa Mbunge huyo, mawakili hao walisema matamshi hayo ya Jalang’o yanadhalilisha jamii hiyo.

Mawakili hao wamesema katika barua iliyopelekewa Jalang’o kwamba alitamka hayo mnamo Jumapili Aprili 27, 2025 alipohutubia waumini katika kanisa la Katoliki la Marani eneo Bunge la Kitutu Chache Kaskani.

Mawakili hao wamedai baada ya matamshi hayo ya kushushia hadhi jamii hiyo, Jalang’o alifanya mkutano wa kuchangisha pesa.

“Matamshi ya kuita jamii ya Abagusii “wachawi” yalipeperushwa katika vyombo vya habari na kuidhalilisha na kuifedhehesha,” mawakili hao walimweleza mwanasiasa huyo.

Mawakili hao wameeleza madai hayo hayana ukweli wowote licha ya madai ya Jalang’o aliwasikia watu fulani wakidai hivyo.

Mwanasiasa huyo ameelezwa kwamba matamshi hayo yanazua chuki ya kijamii na anapasa kuyafutilia mbali.

Iwapo hatayaondoa na kuomba msamaha Bw Omari kupitia kwa wakili Melody Mageto itabidi wamfungulie mashtaka Jalang’o.

Mbunge huyo mawakili wamesema anapasa kuchunga matamshi yake mahala pa umma na hastahili kusema maneno ya kuzua chuki na hisia mbaya za kijamii.

Jalang’o ametakiwa “akome kueneza matamshi kama hayo aidha katika vyombo vya habari ama mitandao yoyote ya kijamii”.

Pia ametakiwa kuheshimu jamii zote nchini.