Handisheki ya Ruto na Uhuru yaporomoka
HANDISHEKI kati ya Rais William Ruto na mtangulizi wake Uhuru Kenyatta, iliyofanyika kwa faragha Ichaweri, Gatundu Desemba mwaka jana ilizua matumaini ya maridhiano baada ya miaka ya uhasama wa kisiasa.
Wakenya wengi walichukulia mkutano huo kama fursa ya viongozi hao wawili kuzika tofauti zao na kulenga maendeleo ya taifa.
Hata hivyo, miezi michache baadaye, hali imebadilika. Kauli ya hivi majuzi ya Rais mstaafu Kenyatta aliyotoa katika Chuo Kikuu cha Makerere, Uganda, imeibua joto jipya kisiasa.
Akiwahutubia viongozi wa vyuo vikuu barani Afrika, Kenyatta aliwahimiza vijana kusimama kidete dhidi ya utawala usiozingatia haki, akiwaita “jeshi la mabadiliko.”
Huu ni wakati wenu. Mna nguvu, mna muda, mna idadi. Msikae kimya mkiona haki zenu zikikandamizwa. Gen Z nyinyi ndio kesho, simameni imara mjitete – Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta
Kauli hiyo imepokelewa kwa hasira na maafisa wa serikali ya Ruto, wakimlaumu kwa kuchochea maandamano na kujaribu kuyumbisha serikali iliyoko madarakani.
Waziri wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen aliongoza mashambulizi dhidi ya Kenyatta.
“Wewe ulikuwa Rais jana tu. Wakati ule hukufanya chochote kwa vijana, leo unataka kuwachochea dhidi ya serikali? Huu ni unafiki wa hali ya juu,” alisema Murkomen.
Naibu Rais Kithure Kindiki naye alitoa tamko kali, akisema:“Tujadili utawala kwa hoja, si kwa uchochezi. Serikali hii itahukumiwa mwaka 2027 kwa kazi yake, si kwa miito ya maandamano.”
Wandani wengine wa Ruto, akiwemo Sylvanus Osoro, walimkosoa Kenyatta kwa kuwa chanzo cha matatizo ya vijana, wakidai aliwafungia milango alipokuwa mamlakani kwa kutoa fursa kwa wazee kama Moody Awori badala ya vijana.
“Wakati wa uongozi wake, vijana walipata kampuni 200 za kamari. Alitufungia milango, leo anatuambia tusimame kidete? Hapana,” alisema Osoro.
Lakini upande wa Kenyatta haujakaa kimya. Wanasiasa wa upinzani wamejitokeza kwa nguvu kumtetea, wakisema kauli zake ni halali na zinalenga kupaza sauti ya vijana waliotamauka.
Mbunge wa Kitutu Chache Kusini, Anthony Kibagendi, alisema wanaomkosoa Uhuru wanaogopa ukweli.
“Wamezoea kusifiwa hata wanapofeli. Uhuru alisema ukweli: vijana hawaridhishwi na serikali hii.”
Mbunge wa Tetu Geoffrey Wandeto aliongeza: “Badala ya kushughulikia matatizo kama bei ya unga na ukosefu wa ajira, serikali inashambulia aliyekuwa Rais. Huu ni udhaifu mkubwa wa uongozi.”
Msemaji wa Rais Ruto, Emmanuel Talam, amedai kuwa maoni ya wanasiasa wa Kenya Kwanza kuhusu Kenyatta ni ya kibinafsi, si msimamo wa Rais.
“Wanasema wanachojua. Rais hana uhusiano wowote na hayo matamshi,” alisema Talam.
Naye msemaji wa Kenyatta, Kanze Dena amesema taarifa rasmi zilitolewa kupitia kurasa za mitandao ya kijamii za rais mstaafu, na hawana cha kuongeza kwa sasa.